IFAHAMU JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA (JWTZ)
Historia
HISTORIA YA JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA
Historia ya kazi na shughuli za ulinzi na usalama hapa Tanzania zilianza tangu zama za mababu zetu. Jamii nyingi zilizoishi katika maeneo mbalimbali hapa nchini zilikuwa na ulinzi wa jadi uliohusisha kila mwanajamii. Ulinzi wa jadi ulikuwa ndiyo msingi wa usalama wa jamii zote kwa wakati ule. Silaha zilizotumika na mababu zetu zilikuwa duni kama vile upinde, mikuki, mundu,mapanga na sime kama silaha za msingi kulinda jamii zao. Kila kabila lilikuwa na namna ya kuwaandaa vijana wao kujifunza matumizi ya silaha na baadaye vijana walipewa jukumu la kulinda jamii zao.
Bara la Afrika lilipata mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii baada ya Mapinduzi ya viwanda yaliyotokea huko Ulaya katika karne ya 19. Mkutano mkuu wa Berlin uliofanyika kuanzia mwaka 1884 hadi 1885 ulifuatiwa na mabadiliko makubwa ya nchi za kiafrika kutawaliwa kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Huu ndiyo mwanzo wa nchi nyingi barani Afrika kuanza kuwa chini ya majeshi ya kigeni.
Ujerumani ilijipatia uhalali wa kuitawala Tanganyika baada ya mkutano wa Berlin ulioligawa bara la Afrika katika vipande vya nchi bila ridhaa ya waafrika wenyewe. Jeshi la Kijerumani lilianzisha harakati za kufuta tawala za makabila mbalimbali hapa nchini ili kuwa na utawala mmoja na jeshi moja la kikoloni. Harakati hizo za Wajerumani zilipelekea baadhi ya makabila kupambana na Jeshi la Kijerumani, kwa vile utawala wa kijerumani ulilenga kuharibu mfumo mzima wa ulinzi wa jadi, siasa na uchumi wa wenyeji.
Vita ya Chifu Mkwawa mwaka 1890 ni mfano kamili unaoonesha kuwa baadhi ya makabila hapa nchini yalikuwa na ulinzi imara japokuwa yalikuwa yanatumia silaha duni. Hata hivyo, miaka michache baada ya Chifu Mkwawa kushindwa vita na Wajerumani, kulianza vita vya majimaji iliyopiganwa kuanzia mwaka 1905 hadi 1907.
Vita hiyo iliiweka historia ya Tanganyika katika ramani ya dunia kwa kuwa makabila mbalimbali yalitumia silaha zao za jadi kupinga uvamizi wa majeshi ya kigeni, lakini kwa umoja wao walisimama kidete kupambana Uafrika wao.
Kipindi hicho cha kuligawa Bara la Afrika kilileta mabadiliko ya kiulinzi na kiusalama kwa vile Waafrika walinyang’anywa haki yao ya kujilinda na ndiyo ukawa mwanzo wa majeshi ya kisasa kuanza kutumika hapa nchini.
Harakati za kijeshi hapa nchini ziliingia katika sura mpya baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kuanzia mwaka 1914 hadi 1918, Wajerumani walipoteza na kunyang’anywa makoloni waliyokuwa wanayatawala kama sharti mojawapo la kushindwa vita. Tanganyika iliwekwa chini ya uangalizi wa Uingereza na kwa udhamini wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, kuanzia kipindi hicho muundo wa Jeshi rasmi lililoongoza Tanganyika lilijulikana kama Kings African Rifles (KAR).
Licha ya KAR kuwa Jeshi la Tanganyika iliyokuwa chini ya Uingereza, bado mfumo wa uandikishaji na ajira Jeshini haukuwa rasmi. Vijana walishirikishwa katika kazi za ulinzi pale walipohitajika. Wakati wa amani vijana walikuwa wakishiriki katika kazi za uzalishaji mali pamoja na shughuli nyingine za kifamilia kama mila na desturi za Kiafrika zilivyoelekeza kwa kila mwanajamii kuishi. Hata hivyo, kwa kipindi hicho cha ukoloni, bado Jeshi la jadi liliendelea kuwepo kwa kila kabila na jamii kwa vile KAR haikuwa kila sehemu ya nchi.
Baadhi ya makabila yalikuwa yamejiimarisha zaidi kiulinzi ukilinganisha na makabila mengine. Kuyataja kwa uchache ni kama vile:- Wahehe, Wanyamwezi, Wasukuma, Wamasai na Wakuria. Hawa walikuwa na mfumo wa ulinzi wa makabila yao.
Kwa mfano, kabila la Maasai walikuwa na mfumo mzuri sana wa kiulinzi. Mafunzo ya ulinzi na usalama ya kabila hilo yalikuwa yanatolewa kulingana na rika na umri wa kijana. Kadhalika, Wasukuma nao walikuwa na mfumo mzuri wa kuimarisha usalama wa kabila lao na ulinzi ambapo walikuwa wakijikusanya katika vijiji ili kutambuana na kuweka mikakati ya ulinzi katika kabila lao. Vijana walikutana kwa ajili ya kujifunza namna ya kulenga na kutupa mishale na mikuki ili kujiweka tayari kwa vita.
Jambo la msingi katika ulinzi wa jamii kabla na wakati wa ukoloni ilikuwa ni jukumu la ulinzi na usalama kuwekwa katika mikono ya kila mwanajamii. Kila mwanajamii aliyekuwa na afya njema alitakiwa kuwa mstari wa mbele kusimamia na kuhakikisha ulinzi wa kila mwanajamii ni jukumu la kila mmoja wao.
Mtemi Mirambo wa Unyanyembe aliamua kupinga ujio wa utawala wa kikoloni mwanzoni kabisa mwa karne ya 19. Uwezo na umahiri wa kijeshi wa makabila mengi hapa Tanganyika ulianza kuonekana wakati wa kupinga ukoloni kabla na baada ya Mkutano Mkuu wa Berlin 1884 hadi 1885 na mwanzoni mwa karne ya 20.
Kiongozi wa kabila la Wahehe Chifu Mkwawa alifanikiwa kupambana na utawala wa Wajerumani kwa takribani miaka mitatu, ambapo mwaka 1891 Mkwawa alishinda. Chifu Munyigumba ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa kabila la Wahehe, kati ya mwaka 1860 na 1880 aliunganisha zaidi ya koo 100 na kuwa chini ya mamlaka ya uongozi wake kitu ambacho kilimfanya Munyigumba kuonekana ndiye kiongozi mahiri wa kabila la Wahehe na alifanikiwa kutetea himaya yake kutoka kwa wavamizi wengine.
Hadi kifo chake, mwaka 1880 Munyigumba alifanikiwa kutetea kabila la Wahehe ambapo baada ya kifo chake Chifu Mkwawa alichukua nafasi na kufanikiwa kusimama imara kupinga uvamizi wa wageni. Jina ‘Mkwawa’ lilitokana na neno ’Mkwavinyika’ lenye maana ya Mteka ardhi kwa kuwa alikuwa na mfumo mzuri wa Jeshi uliomsaidia kutanua himaya yake.
Hata hivyo Chifu Mkwawa aliteua Makao Makuu yake kuwa Kalenga ambapo alijenga ngome yake yenye urefu wa kilomita 13 na ukuta kwenda juu ulikuwa na urefu wa mita 3.5 akaweza kuimarisha kambi za kijeshi na kuhamasisha mbinu nzuri za kilimo kwa watu wake na kufanikiwa kuwa na Jeshi imara ambalo lilikuwa tayari muda wote.
Kutokana na mfumo mzuri aliokuwa nao Chifu Mkwawa, aliweza kuhoji ujio wa wageni na kupigana na Wajerumani waliokuwa na silaha bora lakini aliweza kuwapa changamoto. Kutokana na upinzani wa Jeshi la Chifu Mkwawa,ilipofika Julai 1891, Kamishna wa Kijerumani Emil Von Zelewski aliongoza kikosi cha askari wa kiafrika wapatao 320 kwenda kumvamia Chifu Mkwawa, lakini alishindwa kumdhibiti kwani Jeshi la Mkwawa lilikuwa na askari 3,000 waliokuwa imara. Maafisa na askari wa Jeshi la Kijerumani wote waliuawa kwenye mapigano yaliyotokea eneo la Lugalo-Iringa.
Hata hivyo, tarehe 28 Oktoba 1894, Wajerumani chini ya Kamishna Kanali Friedrich Von Schele walipambana na Mkwawa katika ngome yake huko Kalenga, lakini kiongozi huyo alifanikiwa kutoroka. Baadaye Chifu Mkwawa alianzisha mapigano ya kuvizia hadi Julai 1898 ambapo aligundua kwamba amezungukwa na maadui na kuamua kujiua mwenyewe kabla ya kukamatwa na wakoloni wa Kijerumani.
Vita vya Majimaji ilianzishwa na makabila ya Kusini ambayo yalipinga utawala wa Kijerumani. Vita hii ilianzishwa na Wamatumbi wa eneo la Nandete katika Wilaya ya Kilwa kuanzia July 1905 hadi Agosti 1907. Kiongozi wa vita hiyo alikuwa Kinjekitile Ngwale, maarufu kama Bokero ambaye aliwapa wafuasi wake dawa ya vita ambayo aliwaambia kwamba risasi za Wajerumani zingegeuka kuwa maji.
Askari hao wa Kinjekitile walikuja kwa kasi mpya kwa kipindi hicho ambapo waliendelea kupambana na Jeshi la Wajerumani. Vita hii ilihusisha jamii mbalimbali yakiwemo makabila ya Wangindo, Wandendeule, Wabena, Wamwela na Wangoni. Vita ya Majimaji ilikuwa vita dhidi ya Wajerumani ambao walitawala Tanganyika tangu mwaka 1885 na kunyang’anya ardhi na kuvuruga maisha ya wenyeji.
Pamoja na juhudi za makabila hayo, bado Wajerumani walifanikiwa kuwashinda wapiganaji wa vita vya Majimaji kwa vile walikuwa na silaha bora. Hatimaye, mwisho wa vita ya majimaji viongozi wote wa vita hiyo walikamatwa na kunyongwa na Wajerumani.
Tanganyika ilikuwa chini ya Wajerumani baada ya Mkutano wa Berlin wa mwaka1884 hadi 1885, ulioitishwa na Chancellor Otto Von Bismark wa Ujerumani. Kipindi cha ukoloni, Wajerumani walianzisha kikosi ambacho walikiita kikosi cha kujilinda ambacho kilikuwa na Askari kati ya 2,500 na 3,000 ambao walikuwa na asili ya kiafrika na waliongozwa na Maafisa wanane wa Kijerumani japo wengine hawakuwa Maafisa. Kadiri siku zilivyokuwa zikiendelea waliendelea kuandikisha wananchi na kufikia idadi ya askari 12,000 kabla ya vita ya kwanza ya dunia. Watanganyika walioandikishwa katika Jeshi hilo waliitwa Soldat na wachache wao walifanikiwa kufikia cheo cha koplo.
Mafunzo yaliyotolewa kwa askari wa Kiafrika, yalifuata Mitaala ya Kijerumani na maelezo yake yalikuwa yakitolewa kwa lugha ya Kiswahili ambapo Dar es Salaam ilikuwa ndiyo eneo maalum kwa ajili ya kuandikisha askari wa Jeshi la kikoloni pamoja na mafunzo. Wajerumani waliviweka vikosi vyao katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo Arusha, Kilimatinde Masoko, Ujiji, Bukoba, Tabora, Dar es Salaam, Mahenge, Kondoa na Mwanza.
Hata hivyo, wakati wa utawala wa Wajerumani kulikuwa na vituo mbalimbali ambavyo viliitwa DOMA kabla ya utawala wa Uingereza ambayo ilibadilishwa jina na kuitwa British Overseas Management (BOMA). BOMA zilijengwa katika wilaya kuanzia mwaka 1889 ili kudhibiti ongezeko la watu pamoja na kusimamia shughuli za kiutawala. Vituo hivi viliwekwa kwa lengo la kiulinzi na kulindwa na askari. Baada ya vita vya Chifu Mkwawa na ile ya Majimaji, maboma makubwa yalianzishwa huko Iringa, Mahenge na Songea kwa ajili ya utawala wa Wakoloni.
Wakati wa Vita Kuu ya kwanza ya Dunia mnamo 1914 hadi 1918; koloni la Tanganyika liliendelea kuwa koloni la Wajerumani kwa muda mfupi, ambapo mwaka wa kwanza wa vita vya kwanza vya dunia, Wajerumani walikuwa imara kiasi cha kupenya katika himaya za wenyeji. Kitendo cha Jeshi la Uingereza kuwavamia Wajerumani katika himaya ya Afrika ya Mashariki kilimfadhaisha Jenerali Paul Von Lettoe Vorbeck na hasa baada ya meli kutia nanga katika bandari ya Tanga, mwaka 1914.
Hata hivyo, mbinu za Kamanda huyo wa Kijerumani ziliashiria lengo la kuongeza nguvu ya msaada. Pamoja na hayo, Lettow-Vorbeck alifanya kampeni dhidi ya Waingereza na kufanikiwa kufundisha baadhi ya askari matumizi ya uwanja wa vita na eneo zuri kimapigano pamoja na namna ya kufanya shambulizi la kunuia.
Wake za askari pia walikuwa wakishirikishwa wakati wa mashambulizi. Katika harakati hizo Lettow-Vorbeck alifanikiwa kuongoza askari 15,000 wakiwemo 70 wa silaha za msaada. Askari wote hao walikuwa wanaandaliwa kukabiliana na askari wapatao 160,000 wa himaya ya Waingereza chini ya Jenerali Jan Smuts wa Afrika ya Kusini.
Hata hivyo, mwaka 1916 Smuts alifanikiwa kuteka mipaka ya Kaskazini ambayo iliwekwa chini ya Himaya ya Waingereza. Wakati huo Jeshi la Ubelgiji likiongozwa na Jenerali Charles Tombeur walifika Tabora kutoka mataifa ya Magharibi na kulazimisha kuingia mkoa wa Kagera kwa kutokea Uganda. Uwezo na nidhamu ya kimapigano ya Jeshi alilokuwa nalo Lettow-Vorbeck ulimwezesha kufanikiwa kupigana kwa muda wa miaka minne na hatimaye walishindwa rasmi mwaka 1918 kabla ya kulazimika kurudi Ulaya.
Wakati wa vita ya kwanza ya dunia askari waliokuwa wamechukuliwa Tanganyika baadaye walibadilishwa kutoka Jeshi la Wajerumani lililoshindwa na kuingizwa katika Jeshi la Waingereza lililojulikana kama Kings African Rifles (KAR). Jeshi hilo la KAR lilizidi kupanuka na kujitanua ndani ya shirikisho la Afrika ya Masharika. KAR lilikuwa na vikosi viwili ambavyo askari wake walitokea Tanganyika, Kenya na Uganda na KAR baada ya vita ilikuwa na askari kati ya 400,000 na 500,000 kutoka Afrika Mashariki.
Tanganyika ilishuhudia Waingereza kwa mara ya kwanza katika vita ya kwanza ya dunia baada ya kuishambulia Dar es Salaam kwa mzinga aina ya Mi- ser HMS Astraea na kufanikiwa kuiteka meli ya kibiashara tarehe 08 Agosti 1914. Wajerumani waliamua kuiteka bandari ya Dar es Salaam na kusababisha mapigano makali katika bandari hiyo kitu ambacho mwaka 1916 bandari iliachiwa huru.
Baada ya bandari kupata hitilafu kutokana na mapigano, wafanyabiashara wa Kijerumani na Meli yao ya SMS Konigsberg iliyokuwa inatakiwa kutia nanga Dar es Salaam ilirudi na kuingia kwa kutumia mto Rufiji kwa ajili ya kurekebisha moja ya injini zake iliyokuwa na matatizo. Baadaye tarehe 11 Julai 1915 Waingereza waligundua mahali ambapo SMS Koningsberg ilikuwepo na kuishambulia vibaya katika mto Rufiji na kuizamisha.
Wakati huo huo katika ziwa Tanganyika kulikuwa na mapigano makali kati ya wanamaji Wajerumani, Waingereza na Wabelgiji mwishoni mwa miaka ya 1915 na 1916 walikuwa wakigombea kuchukua mto. Kwa mara ya kwanza meli ya SMS Kingani ilivunjwa na kutekwa ambapo HMS foji ilibadili njia. Mara ya pili meli ya SMS Hedwing Von Wissman, SMS Graf Von Goetzen zilishambuliwa na baadae kupigwa na ndege vita za Wabelgiji na kumalizwa kabisa. Mwaka 1921 ilianza tena kuingia kwenye ukarabati ndani ya ziwa Tanganyika kuanzia mwaka 1927 na kupewa jina la MV Liemba (Graf Von Goetzen). Meli hii ya Liemba bado inafanyakazi mpaka leo hii katika ziwa Tanganyika.
Wageni walijiimarisha zaidi katika fukwe kitu ambacho kiliwafanya Wajerumani warudi nyuma kupitia ziwa Tanganyika na kuwaachia Waingereza na Wabelgiji kutawala. Wananchi wa Tanganyika walihusishwa katika mapigano ya pande zote na ndiyo waliokuwa wakiendesha hizo meli baada ya kupata mafunzo.
Kings African Rifles hapa Tanzania
Baada ya vita ya kwanza ya dunia, mamlaka ya kuongoza Tanganyika yalikuwa chini ya waingereza kwa maamuzi yaliyotolewa na Umoja wa mataifa mapema mwaka 1920 kama sharti la Ujerumani kushindwa Vita Kuu ya kwanza ya dunia. Ofisi ya Mkuu wa himaya ilianzishwa hapa nchini na kupewa jina la Himaya ya Tanganyika. Baada ya kuibuka vita ya pili ya dunia mwaka 1939 kikosi cha 6 cha KAR kilichokuwa Afrika Mashariki kiliandaliwa tayari kwa mapigano baada ya Italia kuingia vitani mwaka 1940.
Askari kutoka Tanganyika walishiriki kikamilifu katika vita kuu ya pili ya dunia kwa upande wa Uingereza. Mapigano kwa mara ya kwanza yalikuwa Somalia ambapo KAR walitembea kilomita 277 na walitumia masaa 53 kutembea kwa miguu kuelekea uwanja wa mapigano wakitokea Kenya hadi Absisinia mnamo mwaka 1940 hadi 1941 na kufanikiwa kuteka Addis Ababa ambayo ilikuwa ndiyo mji wa kivita katika historia.
Hata hivyo pamoja na kikosi cha sita cha KAR kulikuwa na kikosi cha 2 cha Zanzibar kilichohusika na huduma ya kwanza ambacho kilikuwa kikifanya kazi na kikosi cha tiba cha Afrika ya mashariki. Baadaye kikosi hicho kilienda Ceylon na kujiunga na kikosi cha 14 (XIV) ilichokuwa kimeandaliwa ili kupigana katika nchi ya Burma na Jeshi la kutoka Japan. Baada ya vita ya pili ya dunia Tanganyika iliamuriwa kuwa koloni halisi la Uingereza mnamo tarehe 13 Disemba 1946, kuanzia kipindi hicho mambo mengi ya Tanganyika yalianza kubadilika, ikiwa ni pamoja na kuanza harakati za kisiasa na uimarishaji wa Jeshi la Uingereza.
Baada ya vita ya pili ya dunia shughuli za ulinzi na usalama zilikuwa chini ya Uingereza na KAR ilizidi kujiimarisha uwepo wake hapa nchini kwa kuandikisha vijana wa Tanganyika kujiunga na KAR.
Tanganyika Rifles
Tanganyika ilipata uhuru wake tarehe 09 Disemba 1961. Katika sherehe ya uhuru serikali ya Tanganyika ilitangaza kubadili jina la Jeshi la Kings African Rifles (KAR) na kuwa Tanganyika Rifles (TR). Pamoja na jina zuri lililoakisi jina la nchi huru, TR ilibakia na mfumo ule ule wa kikoloni. Kikosi cha sita kilichokuwa katika kambi jijini Dara es Salaaam, Kiliendelea kuongozwa na Luteni Kanali Rowland Mans aliyekuwa mwingereza.
Kikosi cha pili kilichokuwa Kalewa (Mirambo Tabora) kiliendelea kuongozwa na Luteni kanali Harry Martsons mwaka 1963 ambapo alikuwa ni afisa katika Jeshi la KAR. Wakati huo huo, Kombania moja ilipelekwa Nachingwea mnamo mwaka 1963 chini ya Meja Morris Temple ambaye naye alikuwa ni mzungu kwa ajili ya kuanzisha kikosi kipya kilichopewa jina la Gonder kuwapa heshima askari kufuatia ushindi wa KAR walioupata huko Burma.
Zanzibar ilipata uhuru wake kutoka kwa Uingereza tarehe 10 Disemba 1963 baada ya uchaguzi uliokuwa na utata na ndugu Mohammed Shamte alikuwa Waziri Mkuu. Lakini Zanzibar iliendelea kuwa chini ya utawala wa Sultan Jamshid Bin Abdullah aliyeondolewa katika utawala kwa mapinduzi matukufu yaliyofanywa na wananchi wa Zanzibar tarehe 12 Januari 1964.
Mapinduzi yale yalichangiwa na waafrika walio wengi kuupinga utawala wa Sultan Abdullah. Ndiyo maana chini ya Hayati Abeid Amani Karume, waafrika walipindua utawala wa kisultan na Zanzibar ikaongozwa na Baraza la Mapinduzi hadi hii leo.
Aidha, pamoja na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar viongozi wa pande zote mbili za Tanganyika na Zanzibar walifanya maamuzi ya busara mnamo tarehe 26 Aprili 1964. Tanganyika iliungana na Zanzibar na kuwaJamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwa taifa moja. Kufuatia Muungano wa nchi mbili hizi ulijumuisha mambo kumi na moja kuwa ya muungano na kati ya hayo mambo ya Ulinzi yalijumuishwa katika muungano. Kwa hiyo ni dhahiri kuwa majeshi ya nchi mbili hizi yaliunganishwa rasmi tarehe 24 July 1964.
Januari 1964 ulikuwa ni mwaka muhimu sana katika historia ya siasa ya Tanzania kwani ndiyo mwaka ambao askari wa Jeshi la Tanganyika Rifles walifanya maasi tarehe 20 Januari 1964. Na ndiyo mwaka ambao TR ilivunjwa rasmi tarehe 25 januari 1964 na kupelekea Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kuzaliwa rasmi tarehe 01 Septemba 1964. Mabadiliko yaliyotokea Tanganyika yalitokea Zanzibar japo kwa namna tofauti.
Tarehe 12 Januari 1964 Jeshi la Ukombozi la Zanzibar lilizaliwa na katika mchakato wa kuunganisha nchi mbili hizo, Jeshi hilo liliungana na Tanganyika Military Force kwa muda na hatimaye kuunda Jeshi jipya lililopewa jina la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Maasi ya tarehe 20 Januari 1964 yalianzia Collito Barracks (Lugalo Dar es Salaam) na baadaye kuenea hadi Kalewa Barracks iliyokuwa Tabora. Hata hivyo maasi hayakuishia Tabora bali hata Kombania mpya iliyokuwa imepelekwa Nachingwea, kwa maandalizi ya kuanzisha kikosi kipya cha tatu hapa Tanzania nayo askari wake walijiingiza katika maasi hayo. Zipo sababu mbalimbali ambazo zimeelezwa kuwa zilikuwa ni chanzo cha maasi ya Januari 20.
Kutokana na hotuba ya Amiri Jeshi mkuu na Rais wa Tanganyika wakati huo kupitia redio ya taifa, Mwalimu Nyerere aliwaambia Wananchi kuwa Wanajeshi walikuwa na madai mbalimbali kuwa sababu za maasi ilikuwa ni pamoja na, Askari waafrika walitaka kuharakishwa kwa sera ya africanization ndani ya Jeshi la Tanganyika Rifles ili maafisa na askari wazungu waondolewe jeshini ili Wafrika maafisa na askari waongoze Jeshi lao la Tanganyika huru.
Sababu nyingine iliyokuwa kero kwa askari hawa wa TR ilielezwa kuwa ni nyongeza za mishahara. Mishahara ililipwa kwa madaraja ambapo maafisa na askari waafrika walilipwa mishahara ya chini ukilinganishwa na mishahara waliyolipwa maafisa na askari wa kizungu ilikuwa juu zaidi ya mishahara ya waafrika. Kulikuwa na madai ya askari kutaka kuboreshewa maisha na mazingira ya kazi. Hata hivyo, baada ya mazungumzo yaliyoendeshwa na Waziri wa Mambo ya nchi za nje na ulinzi Mheshimiwa Oscar Kambona, Serikali ilikubali kuongeza mishahara na kuboresha mazingira ya kazi.
Wakati maasi yakitulizwa kwa mazungumzo serikali ilifanya jitihada za kuomba msaada wa majeshi ya Uingereza kuja nchini kuzima maasi hayo. Serikali ya Tanganyika iliamua kuomba msaada kutoka serikali ya Uingereza kwa vile ingekuwa rahisi kwao kuja kwani maafisa na askari wao walikuwa wanashikiliwa na askari waliofanya maasi. Sababu nyingine ya kuwaita Uingereza kuja kumaliza mgomo, itakumbukwa kuwa bado Tanganyika Rifles ilikuwa inaongozwa na maafisa na askari viongozi wa Uingereza. Mkuu wa Majeshi ya Tanganyika wakati wa maasi alikuwa ni Brigedia Jenerali Doglous kutoka Uingereza.
Baada ya maasi kuzimwa kwa msaada wa Makomandoo wa Uingereza, viongozi wote walioshiriki kuwashawishi wenzao kushiriki katika maasi walifukuzwa Jeshini. Viongozi na vinara wa maasi wengine walifunguliwa mashitaka ya uasi. Wale maafisa na askari viongozi ambao hawakushiriki katika maasi walibakizwa jeshini kwa muda na Jeshi lilibadilishwa jina kutoka Tanganyika Rifles na kuitwa Tanganyika Military Force. Jina hilo lilidumu kwa muda mfupi hadi Jeshi jipya lilipozaliwa tarehe 01 Septemba 1964 na kupewa jina la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, jina linalotumika hadi leo.
Njia zilizotumiwa na wakoloni kuwaandikisha wanajeshi ili kuwa ni zile za kupita kijiji hadi kijiji kupima afya za vijana na kupima urefu kwa ajili ya kuwaandikisha jeshi. Lakini baada ya serikali kuvunja Jeshi la Tanganyika Rifles kutokana na maasi hayo, Amiri Jeshi mkuu na rais wa Tanganyika Mwalimu Julius Nyerere alitoa mwito kwa vijana wa TANU Youth Leaque wajiandikishe katika ofisi za TANU kwa ajili ya kuunda Jeshi jipya, Vijana wengine waliokuwa katika Jeshi la Kujenga Taifa nao waliandikishwa katika Jeshi jipya.
Tofauti na njia zilizotumiwa na wakoloni kuandikisha vijana jeshini, vijana walioandikishwa katika Jeshi jipya ni wale tu waliokuwa wazalendo na waaminifu kwa nchi yao. Vijana wanachama wa TANU walipewa umuhimu katika Jeshi jipya kwa vile chama hicho kilikuwa kimeenea nchi nzima na kilikuwa Chama cha Wazalendo.
Mafunzo kwa askari wa jeshi jipya yalianza rasmi katika kambi ya Mgulani tarehe 03 Machi 1964 hadi walipomaliza mafunzo yao ya awali tarehe 01 Septemba mwaka huohuo. Askari wapatao 1,000 walikula kiapo mbele ya Amiri Jeshi mkuu na Rais wa Tanzania Mwalimu Julius Nyerere na Katika sherehe hizo Rais Abeid Amani Karume aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo pia alihudhuria.
Askari hao wapya walimaliza mafunzo yao ya awali na kuingizwa rasmi katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Huo ulikuwa mwanzo na safari ndefu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania la sasa.
Aidha, harakati za kuliimarisha Jeshi jipya zilianza kwa kasi kubwa mara tu baada ya uhuru, ili kufikia malengo ya nchi kuwa na Jeshi lake. Mafunzo kwa maafisa yalifanyika kwa muda katika nchi rafiki, kama vile Canada, Uingereza, Israeli, India, China na Pakistan. Tanzania ilitaka kujitegemea kwa kuwa na Jeshi lake lenyewe.
Kutokana na hitajio kwa maafisa na askari wenye ujuzi na waliofunzwa vizuri serikali ya Tanganyika kwa wakati ule iliamua kupeleka askari wengi nje ya nchi kufanya mafunzo ya uafisa kadiri serikali ilivyoweza. Ilikuwa ni gharama kupeleka askari nje lakini hitajio lilikuwa kubwa na nchi ililazimika kuendelea kuimarisha Jeshi kwa haraka na ilibidi kwa hali yoyote ile vijana hao wapelekwe huko ili kupata maafisa wengi kwa haraka.
Itakumbukwa kuwa kabla na baada ya kupata uhuru nchi ilikuwa na nafasi ya kupeleka afisa mwanafunzi mmoja kila mwaka nchini Uingereza kupata mafunzo, hatua ambayo ingeichukua Tanzania miaka hamsini kupata maafisa hamsini. TANU ilitumia mbinu nyingine na kupeleka vijana 15 wa TANU kufanya mafunzo ya uafisa nchini Israeli mwaka 1963.
Baada ya kuanzishwa kwa JWTZ, Jeshi liliendeleza vikosi vile vile vitatu vya askari wa miguu ingawa majina yalibadilishwa ili kulipa Jeshi taswira ya kufanana na mazingira ya Tanzania huru na kambi hizo zilizokuwa zinatumia majina ya kigeni, kuanzia wakati huo zilipewa majina ya kizalendo kama; Collito Barracks ilipewa jina Lugalo kwa ajili ya kumbukumbu ya Chifu Mkwawa wa Iringa alivyopambana na Wajerumani na kuwaua katika eneo la Lugalo. Kambi ya Kalewa Tabora ilipewa jina la Chifu Milambo kwa ajili ya kumuenzi kwa jinsi alivyosimama imara kupinga ukoloni.
Dira, Dhima na Majukumu
JESHI LA ULINZI LA WANANCHI WA TANZANIA (JWTZ)
JWTZ lilianzishwa tarehe 01 Septemba 1964 likiwa na lengo la kulinda uhuru wa nchi na mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dira ya JWTZ
Kuwa na Jeshi dogo, shupavu la Viongozi na Wataalamu wenye zana na silaha za kisasa, utayari wa hali ya juu katika ulinzi wa nchi ya Tanzania.
Dhima ya JWTZ
Kulinda nchi na kutetea maslahi ya Taifa la Tanzania, kutoa msaada kwa Mamlaka za kiraia na kuwezesha kufikiwa kwa malengo ya Kitaifa na Kimataifa.
Majukumu ya Msingi ya JWTZ
• Kulinda Katiba na Uhuru wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
• Ulinzi wa Mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
• Kufanya Mafunzo na Mazoezi ili kujiweka tayari Kivita wakati wote.
• Kufundisha umma shughuli za Ulinzi wa Taifa.
• Kushirikiana na Mamlaka za Kiraia katika kutoa misaada ya kibinadamu na uokoaji wakati wa maafa.
• Kukuza elimu ya kujitegemea na uzalishaji kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
• Kushiriki katika shughuli za Ulinzi wa Amani Kimataifa
KAMANDI ZA JWTZ
Kamandi ya Wanamaji
KAMANDI YA JESHI LA WANAMAJI
Historia ya Kamandi
Kamandi ya Wanamaji ni kati ya Kamandi tatu zinazounda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Kamandi ilianza wakati wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa Jeshi la kisasa lenye mtazamo wa kizalendo wa kuwalinda wananchi wake.
Kamandi ya Jeshi la Wanamaji ilianzishwa rasmi mnamo tarehe 06 Disemba1971, baada ya nchi kuhitaji kuwa na ulinzi wa mipaka yake kwa upande wa bahari ya Hindi, Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa. Maeneo yote hayo ni mipaka ya Tanzania na nchi jirani zinazoizunguka Tanzania. Katika Bahari ya Hindi Tanzania inapakana na Comoro, Shelisheli na Madagascar. Katika Ziwa Victoria Tanzania inapakana na Kenya na Uganda, katika Ziwa Nyasa Tanzania inapakana na Malawi na Msumbiji na katika ziwa Tanganyika Tanzania inapakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi.
Jitihada na juhudi za ziada zilizofanywa na serikali na Makamanda wa Jeshi zilizaa matunda na kufanikiwa kuanzisha Kamandi ya Wanamaji. Jiwe la msingi la kuanza kujenga miundombinu ya Jeshi la Wanamaji liliwekwa na aliyekuwa Rais wa kwanza na Amiri Jeshi Mkuu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere tarehe 06 Disemba 1970 na kukamilika baada ya mwaka mmoja kwa msaada wa Jamhuri ya Watu wa China. Miundombinu iliyojengwa ni pamoja na majengo, karakana, sehemu za kuegesha meli na barabara.
Wanajeshi wa kwanza wa Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania walipata mafunzo yao ya Wanamaji nchini China na baada ya hapo wengine walipewa mafunzo kwa awamu ambapo wataalam wa Kichina wamekuwa wakija Tanzania na wakati mwingine Wanamaji wetu huenda mara kwa mara nchini China kwa ajili ya mafunzo na kubadilishana uzoefu. Kutokana na serikali ya Tanzania kuwa na sera nzuri ya mambo ya nje, Tanzania imekuwa na marafiki wengi wanaotoa nafasi kwa Kamandi kupeleka mabaharia wengine katika nchi zao ili kufanya mafunzo na kubadilishana uzoefu. Nchi hizo ni pamoja na India, Misri, Pakistani na Afrika Kusini.
Wakati Kamandi ya Jeshi la Wanamaji inaanzishwa, ilianza kama kikosi kilichokuwa kinaitwa NAVY FLOTTILA kikiwa na kombania za mapigano pamoja na Kiwanda, Utawala, Kikundi cha Umeme na ile ya Rada. Hii kombania ya Rada ilikuwa na viteule sehemu mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Tanzania visiwani. Makao Makuu ya Kamandi yaliwekwa kwa muda katika eneo la Wazo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Idadi ya meli zilizokuwepo wakati huo zilikuwa 13 ambapo Meli za kivita zilikuwa kumi na nyingine tatu zilikuwa za utawala. Meli za kivita zilikuwa katika makundi mawili, kundi la kwanza ni Gun Boats, lililokuwa na meli sita na kundi la pili ni Topido ambalo lilikuwa na Meli nne. Katika meli nyingine tatu ilikuwepo boti ya mawasiliano yaani ‘topido recovery boat na tag boat'.
Madhumuni ya Kuanzishwa Kamandi ya Wanamaji
Kuanzishwa kwa Kamandi ya Wanamaji ilikuwa ni jambo muhimu la kimkakati kwa ajili ya kuendelea kuhakikisha kuwa mipaka yote inakuwa salama.
a. Kukamilisha muundo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kuwa kila nchi yenye Bahari, Maziwa na Mito mikubwa inahitaji Kamandi ya wanamaji ili kusimamia ulinzi wa maeneo hayo.
b. Kuhakikisha mipaka yote katika Bahari, Maziwa na Mito mikubwa inakuwa salama wakati wote.
c. Kuwapa ulinzi wa kutosha Wananchi wanaoishi kwa kujishughulisha na uvuvi Baharini, Maziwa na mito mikubwa ili waweze kujipatia kipato chao na kuinua uchumi wa Tanzania.
Kuwa Kamandi Kamili
Ujenzi wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji uliendelea kwa malengo ya kupata Kamandi kamili inayoweza kujitegemea katika kudhibiti mipaka yote ya Bahari, Maziwa na Mito. Kadiri muda ulivyokuwa ukienda mabadiliko yalikuwa yakitokea katika kikosi hiki cha Wanamaji, hadi ilipofika mwaka 1983, Serikali ilikuwa imewekeza na kuhakikisha Kamandi ya Jeshi la Wanamaji nchini Tanzania imeanza kufanyakazi kama ilivyokusudiwa. Uanzishwaji wa Kamandi ya Wanamaji ulienda sambamba na kuzibadilisha Kombania kuwa vikosi chini ya Kamandi hiyo ili kuzipa mamlaka kamili ya kiutendaji kama Kamandi ya Wanamaji.
Kombania ya utawala ikaitwa kikosi cha utawala ambacho ndicho kikosi cha Makao Makuu ya Jeshi la Wanamaji kikiwa na kazi ya kuratibu shughuli zote za utawala zinazoihusu kamandi. Kombania ya Lojistiki nayo ikawa kikosi cha Utawala ambacho Majukumu yake makubwa ni shughuli zote zinazohusu ununuzi, usambazaji na usafirishaji wa mahitaji ya vifaa vya Kamandi ya Wanamaji.
Kamandi ya Wanamaji inayo Shule ya Kijeshi ya Ubaharia iliyoanzishwa mwaka 1979 ikiitwa Training Wing hadi mwaka 1980, ilipobadilishwa jina na kuitwa SKU. Shule hiyo ni sehemu ya juhudi za Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kujitegemea kwa kuwajengea uwezo watendaji wake.
Kamandi iliendelea kukua na mwaka 1991 iliongeza ujenzi wa majengo ya Shule kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa maafisa na askari ili kukidhi hitajio la mabaharia hapa nchini. Pia ujenzi wa mwaka 1991 ulienda sambamba na kuwa na vifaa vingi vya kisasa viliongezwa ili kukidhi haja ya sayansi na teknolojia ya kisasa. Shule ya mabaharia imekuwa injini ya Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, mafunzo ya ulinganifu hufanyika kwa ajili ya maafisa ambao hufanya kozi na mafunzo yao katika Kamandi ya Jeshi la Wanamaji na kutoka Kamandi nyingine ili kuleta ufanisi, mafunzo hayo ni muhimu kwa maafisa na askari wanaomaliza mafunzo ya awali kutoka vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Huduma za Kijamii
Kamandi ya Jeshi la Wanamaji imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza sera ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kuweka maslahi ya wananchi mbele. Kamandi imekuwa ikitoa huduma ya afya bure kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya kambi.
Pamoja na huduma za afya kuna huduma ya elimu inayotolewa na Kamandi kwa vijana wanaoishi jirani na shule ya sekondari Kigamboni. Wanafunzi wengine wanatoka mbali kwenda kusoma pale na wamekuwa wakifaulu vizuri na kuchaguliwa kujiunga na masomo ya elimu ya juu.
Huduma zote hizo za kijamii zinatolewa kwa wanajeshi na familia zao, watumishi wa umma na jamii inayoizunguka Kamandi. Madhumuni ya kuanzishwa kwa shule ya sekondari Kigamboni ilikuwa ni kwa ajili ya Wanajeshi wenyewe ambao walihitaji kujiendeleza kielemu lakini pia na kuwasomesha watoto wao, ikiwa ni pamoja na watumishi wa umma na hata watoto wa jamii inayoizunguka kamandi.
Kamandi ya Wanamaji imewahi kuongozwa na makamanda mbalimbali kwa nyakati tofauti kwa mafanikio makubwa.
Meja Jenerali (mstaafu) Rowland L Makunda aliteuliwa kuongoza Kamandi kuanzia mwaka 1971 hadi 1983. Meja Jenerali (mstaafu) Rowland L Makunda alikuwa na historia ndefu katika Kamandi ya Wanamaji, alianza kuongoza Kamandi wakati bado ilikuwa ni kikosi tu cha wanamaji.
Meja Jenerali Rowland Makunda ana historia ya kipekee ambapo ndiye aliyekuwa kiongozi wa maonesho ya kikundi cha utimamu wa mwili (Fitness Training Display) siku Tanganyika inapata uhuru kutoka kwa mkoloni na vilevile alishiriki kikamilifu katika vita ya Kagera.
Meja Jenerali (mstaafu) Ligate Sande aliteuliwa kuongoza Kamandi kuanzia mwaka 1983 hadi 2002 alipostaafu utumishi Jeshini.
Brigedia Jenerali (mstaafu) Joachim Lisakafu aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuanzia mwaka 2002 hadi 2006 alipostaafu utumishi Jeshini kwa umri.
Meja Jenerali (mstaafu) Said Omar aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuanzia mwaka 2006 hadi 2013 alipostaafu utumishi Jeshini kwa umri.
Brigedia Jenerali Rogastian Lasway aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la wanamaji kuanzia mwaka 2013. Alipandishwa cheo na kuwa Meja Jenerali na kuteuliwa tena kuendelea kuongoza Kamandi hiyo hadi 2016.
Rear Admiral Richard Makanzo aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuanzia Aug 2016 hadi Aug 2021.
Rear Admiral Michael Mumanga aliteuliwa kuongoza Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuanzia Aug 2021 hadi sasa.
Wajibu Mwingine wa Kamandi ya Wanamaji kwa Karne hii.
Kamandi ya Jeshi la Wanamaji imetoa mchango mkubwa katika jitihada za kimataifa za kupambana na uharamia katika bahari ya Hindi. Miaka ya hivi karibuni Dunia imekumbana na changamoto za uharamia katika bahari ya Hindi. Sehemu kubwa ya changamoto hizo za uharamia baharini zimetokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe inayoendelea nchini Somalia. Kwa hiyo wapiganaji wanatafuta njia za kupata pesa ili kuendelea na vita hiyo. Njia mojawapo wanayotumia ni pamoja na kuendesha uharamia wa kuteka Meli zote zinazopita katika Pwani ya Afrika Mashariki.
Wanamaji wa Tanzania wanasaidia jitihada za kuzuia uharamia katika Pwani ya Tanzania na Pwani ya Afrika Mashariki. Jitihada hizo za Wanamaji zina lengo la kulinda Meli za kibiashara, pamoja na shughuli nyingi za kiuchumi zinazofanyika katika Bahari ya Hindi kwa kuwa zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa za biashara husafirishwa kwa njia ya bahari.
Aidha, uharamia ukiachwa uendelee utaathiri usafiri wa njia ya Bahari ya Hindi na nchi zitakazoathirika na uharamia ni pamoja na nchi zote zinazotumia bandari ya Dar es Salaam za Zambia, Rwanda, Malawi, Uganda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hivyo uharamia una madhara makubwa kwa maendeleo ya kiuchumi kwa ukanda huu na dunia kwa ujumla.
Jeshi la Wanamaji wa Tanzania limekuwa likifanya doria inayotoa mchango mkubwa katika jitihada za kikanda na za ulimwengu katika kutokomeza uharamia baharini. Msako wa maharamia umekuwa na mafanikio makubwa kwa vile Wanamaji wamekuwa wakishirikiana na majeshi ya nchi rafiki kama Jeshi la Wanamaji wa Afrika Kusini katika kuendesha msako huo.
Itakumbukwa kuwa ilipofika mwishoni mwa mwaka 2003, vyombo vingi vya baharini vilianza kuripoti kuhusu maharamia wa kisomali waliokuwa wakiteka Meli nyingi katika ukanda wa Ghuba ya Aden na maeneo mengine ya bahari ya Hindi. Baada ya Meli kuanza kupita Bahari Kuu, maharamia nao walisogeza mitego yao katika pwani ya Afrika Mashariki na kwa Tanzania mwaka 2010 matukio 18 yaliripotiwa katika kipindi cha miezi kumi (10).
Mwaka huohuo, iliripotiwa kwamba maharamia wamekuwa wakiendeleza uharamia huo umbali wa kilometa 1,850 katika bahari ya Hindi ili kukwepa doria zinazofanywa na vikosi vya wanamaji katika maeneo yao ya utekaji ya awali. Maharamia wamekuwa wakiteka meli jirani zaidi na India kuliko Pwani ya Afrika kwa vile Meli zilikuwa zinapita Bahari Kuu ili kukwepa mitego ya maharamia hao.
Tishio la maharamia wa kisomali katika pwani ya Tanzania kwa meli zinazoelekea bandari ya Dar es Salaam yalihusu makundi ya vijana wanaokadiriwa kuwa 1,500 ambao walikuwa wakizunguka katika pwani ya Afrika Mashariki kwa malengo ya kuteka Meli za biashara. Wengi wa vijana hao wa kisomali walibainika kuwa na umri kati ya miaka 20 na 35 baada ya kukamatwa na kuhojiwa, waligundua kuwa wengi wa vijana hao walikuwa wavuvi hivyo wana ufahamu wa bahari na huutumia ufahamu huo kuzisaka meli baharini. Wanamgambo na wapiganaji wa vita nchini Somalia nao hushiriki kikamilifu katika kuteka Meli kwa vile wana silaha za kisasa zinazowawezesha kutekeleza uhalifu huo.
Aidha, kuna hali inayoonesha kwamba kuna ushiriki wa watalaamu wa simu za satellite, global position system (GPS) na matumizi ya teknolojia nyingine zenye uwezo mkubwa wa kujua mwelekeo na mahali ilipo meli, ushirikiano huo wa maharamia hukamilisha muundo wa vikosi kamili vya utekaji meli baharini.
Uharamia katika bahari ya Hindi, pwani ya Tanzania umekuwa ukitumia mbinu zinazotumiwa katika maeneo mengine katika bahari ya Hindi ambapo boti ziendazo kasi hubeba maharamia watatu hadi saba na kawaida huziteka meli kwa kutumia silaha nyepesi na ndogo, silaha nzito kama bunduki za rashasha (Machine guns), na wakati mwingine hubeba hata roketi na silaha za kupambana na vifaru (RPG). Meli zinazotekwa hupelekwa eneo la Pwani ya Somalia ambapo huhitaji fedha taslimu za kugomboa meli hizo zikiwa na mateka katika eneo zinaposhikiliwa.
Mazungumzo ya kuzigomboa hizo meli hufanyika nje ya Somalia kwa kuwashirikisha watu wenye mawasiliano na watekaji wa meli. Pamoja na kuteka meli hizo, maharamia huwatumia mabaharia na wafanyakazi wengine wa meli zilizotekwa kama ngao pindi wanaposhambuliwa na meli za kivita au waokoaji wa Kimataifa na hivyo hufanya kazi ya uokoaji kuwa ngumu.
Kutokana na juhudi za kimataifa katika kukabiliana na uharamia kufanikiwa kwa kiasi kikubwa, maharamia wamebadili mbinu na aina ya meli wanazoziteka, awali walikuwa wakiziteka meli za uvuvi au meli ndogo za mizigo, siku hizi hulenga meli za kemikali, boti kubwa za uvuvi, meli kubwa za mizigo na hata meli za kifahari za kitalii.
Meli ya mizigo ya MV Asphalt venture iliyokuwa ikisafiri kutoka Kenya kwenda Afrika Kusini mnamo Septemba 2010 ilitekwa umbali wa kilometa 180 kusini mashariki mwa jiji la Dar es salaam. Baada ya kutekwa meli hiyo ilibadili mwelekeo ghafla kutoka ule wa awali kuelekea Durban na kuanza kuelekea pwani ya Somalia, pia meli hiyo ilikuwa haijibu miito ya radio za mawasiliano. Baada ya kuwa mateka kwa miezi kadhaa wafanyakazi wachache kati ya 15 wa meli hiyo waliachiwa huru baadhi waliendelea kushikiliwa. Katika hali isiyo ya kawaida maharamia walikuwa na madai ya ziada, ingawa fedha za kugombolea mateka zililipwa, maharamia hao waliendelea kudai kuachiwa huru kwa maharamia 100 wa Kisomali waliokamatwa na Serikali ya India.
Maharamia hutumia Meli za uvuvi wanazoziteka kama meli mama kwa ajili ya kuwezesha uharamia sehemu mbalimbali ambapo ni mbali na Pwani ya Somalia kwa mfano, Pwani ya Dar es Salaam na maeneo mengine mbali na Pwani ya Somalia. Meli hizi zina urefu wa mita 30 na zinaweza kuchukua watu zaidi ya ishirini (20), Jahazi moja liliwahi kukamatwa na kamandi ya Jeshi la Wanamaji wa Tanzania mnamo mwaka 2010 likiwa na maharamia 10 na wafanyakazi saba (7). Boti ya mwendo kasi inayotumika kwa ajili ya utekaji nyara inaweza kuhifadhiwa na kufichwa katika meli kubwa na kutumika wakati wa uvamizi wakati wa utekaji meli. Meli hizi pia zina uwezo wa kuhifadhi vifaa na chakula, hivyo kuwawezesha maharamia kuishi muda mrefu Baharini.
Pia Jeshi la Wanamaji wa Tanzania limekuwa likikabiliana na tishio la kutaka kutekwa kwa vituo na vifaa vya utafiti wa mafuta na gesi na maharamia katika Pwani ya Bahari ya Hindi.
Kwa sasa maharamia wamepanua maeneo ya utekaji wa Meli wakilenga meli za utafiti na uchimbaji wa mafuta unaofanywa katika bahari ya Hindi kusini mwa Tanzania eneo la Mtwara. Mashambulizi dhidi ya meli za utafiti mwaka 2010 yanabainisha kwamba maharamia walilenga kuwateka wataalamu wanaofanya kazi ya utafiti wa mafuta katika miamba ya bahari.
Kamandi ya Jeshi la Wanamaji imeendelea kuendesha doria za mara kwa mara na kuwawezesha wawekezaji kuwa na imani na usalama wao. Bila hatua madhubuti za kupambana na uharamia huo ingepelekea kukwama kwa mipango mizuri ya serikali katika kuhakikisha kuwa utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi unafanyika katika mazingira salama.
Wawekezaji wamekuwa na jukumu la kuwalipa walinzi katika eneo lao la utafiti dhidi ya maharamia. Kimsingi athari za uharamia zimekuwa kubwa na zimeathiri sekta mbalimbali. Maharamia katika ulimwengu huu wamekuwa wakilipwa mamilioni ya dola za kimarekani na makampuni ya meli zinazotekwa.
Aidha, kutokana na uharamia baharini malipo ya bima kwa usafirishaji wa bidhaa kupitia bandarini zimeongezeka. Meli zimekuwa zikilazimika kuzunguka umbali mrefu ili kukwepa maeneo yanayofahamika kuwa na maharamia. Mzunguko kupitia Afrika Kusini katika rasi ya Tumaini Jema, umekuwa ukichelewesha mizigo inayohitajika kwa haraka na nchi zinazotegemea bandari ya Dar es salaam.
Kutokana na hali ilivyo, maharamia wanavuruga mfumo wa biashara ya usafirishaji baharini ambayo inategemewa katika uchumi wa dunia kwa asilimia kubwa na matokeo yake ni kushuka kwa uchumi au pato linalotokana na biashara hizo. Ongezeko la gharama za usafirishaji hugharimiwa na mteja wa usafiri huo na hivyo kuchangia ongezeko la bei ya bidhaa kwa watumiaji wa bidhaa hizo.
Ongezeko la gharama za usafirishaji mizigo hususani yenye rasilimali kama mafuta, huduma za ukuaji wa uchumi kutokana na ukweli kuwa bidhaa hiyo ndiyo kichocheo pekee cha maendeleo ya uchumi popote duniani. Misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Somalia walio katika mateso ya vita ya muda mrefu ipo mashakani na wakati mwingine hulazimika kupitia nchi jirani ili kuwafikia wahanga wa vita hiyo. Kuna uwezekano mkubwa kuwa siku moja meli ya mafuta inaweza kushambuliwa na kusababisha madhara makubwa kwa mazingira, viumbe wa baharini na ukanda mzima wa pwani ya Afrika Mashariki kuchafuka.
Kamandi ya Jeshi la Wanamaji wa Tanzania linashiriki katika jitihada za kidiplomasia, kimahakama na kisheria ili kuhakikisha kuwa kuna utatuzi wa tatizo la uharamia katika Pwani ya Afrika Mashariki na duniani kote. Tanzania inaendelea kuunga mkono jitihada za Kimataifa za uundwaji wa Serikali yenye mamlaka nchini Somalia na aliyekuwa mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika nchi ya Somalia ni Mwanadiplomasia Mtanzania Ndugu Augastin Mahiga ambaye amemaliza muda wake hivi karibuni.
Lengo ni kupata Serikali itakayosimamia usalama wa pwani na bahari dhidi ya uharamia na kuwasaidia vijana wa kisomali kupata ajira na kuwa na vyanzo halali vya mapato. Ushiriki wa Tanzania katika ulinzi wa bahari na hasa katika ngazi ya kanda umezidi kuimarika kwa vile nchi jirani katika ukanda wa Afrika Mashariki na nchi wanachama wa Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) zinashirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha ukanda huu unakuwa salama wakati wote.
Meli za kivita za Kamandi ya Jeshi la Wanamaji zina mfumo wa kisasa wa mawasiliano. Teknolojia hiyo ya mawasiliano inarahisisha mawasiliano kati ya meli moja na nyingine kuwa ya uhakika. Kamandi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwafukuza maharamia mbali na pwani ya Tanzania na wakati huo huo nyendo za maharamia zimekuwa zikifuatiliwa na Jeshi la Wanamaji kutoka Jumuiya ya Ulaya. Jitihada za kupambana na uharamia katika Kamandi ya Wanamaji zinawashirikisha Polisi wa Tanzania, hiyo yote imetokana na kutungwa kwa sheria kali dhidi ya maharamia. Meli za vikosi hivyo zinaweza kuwakamata na kuwafungulia mashtaka maharamia bila kujali walikamatwa wapi.
Sheria ya uharamia inatoa ujumbe kwa watu wote wanaojihusisha na uharamia kukamatwa na kushitakiwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa dhidi ya uharamia. Kamandi ya Wanamaji wa Tanzania walipambana na maharamia baharini kwa siku nzima mnamo Septemba 2010 ambapo boti ya Wanamaji ilishambuliwa wakati ilipokuwa inapambana na maharamia 50 waliokuwa na silaha. Wanamaji wawili (2) wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walijeruhiwa katika pambano hilo, Wanamaji wa Jeshi wakishirikiana na Polisi walifanikiwa kumkamata haramia mmoja. Katika tukio lingine mwezi huohuo, Wanamaji wa Tanzania walikuwa katika meli ya utafiti wa mafuta walifanikiwa kuwashambulia maharamia waliokuwa wakijaribu kuteka meli hiyo.
Operesheni za baharini zimekuwa zikiungwa mkono na ushirikiano wa Kimataifa katika doria na ukusanyaji taarifa za Kiintelijensia. Meli za mizigo zimekuwa zikihimizwa kuzingatia mbinu bora za usimamizi na uendeshaji wa biashara zao. Meli za Kijeshi za Tanzania na Wanamaji wa nchi za Jumuiya ya Ulaya zilipewa tahadhari kuhusu hali ya Meli ya MV Mississippi Star mnamo Septemba 2010 baada ya kushambuliwa na maharamia Kaskazini Mashariki mwa Jiji la Dar es salaam. Maharamia walikuwa wakitumia bunduki za rashasha na mabomu ya kutupa kwa mkono, maharamia walishindwa kuiteka meli hiyo ya mafuta baada ya nahodha wa meli kuongeza mwendo kasi na kuwapiga chenga kuepuka mashambulizi.
Usalama wa bahari ya Hindi katika pwani ya Tanzania unaimarika siku hadi siku kwa kuongeza uwezo wa Wanamaji wa JWTZ katika kupambana na uharamia. Pia JWTZ linashirikiana na Makampuni yanayofanya utafiti wa mafuta na gesi ili kulinda sekta hii muhimu ya uchumi nchini. Aidha, JWTZ limeanzisha ushirikiano wa karibu na kampuni za usafirishaji baharini na mawakala wa meli ili kuweza kupambana kikamilifu na maharamia. Meja Jenerali Omar Said (sasa mstaafu) aliyekuwa Mkuu wa Kamandi ya Wanamaji alibainisha kwamba ukanda wa pwani ya Tanzania wenye kilometa 800 unapaswa kuwekwa kwenye kampeni maalumu ya kupambana na uharamia. Taarifa za kiintelijensia zinabainisha kwamba maharamia wa Kisomali wanaweza kuweka kambi katika fukwe zinazofikika kirahisi.
Kambi moja ya maharamia iliyotelekezwa iligunduliwa na wanamaji wa Tanzania mwaka 2010 Mkoani Lindi, Kusini Mashariki mwa Tanzania. Lakini pia msako unaendelea ili kubaini kambi nyingine popote zilipo katika ukanda wa Pwani yetu. Tanzania kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama inafanya kazi hiyo kuwa endelevu, Kamandi ya wanamaji inaendelea kushirikiana na jumuiya ya Kimataifa katika nyanja za kiintelijensia na kuhakikisha usalama wa vyombo vinavyotumika majini na hasa baharini unakuwepo wakati wote.
Mafanikio ya Wanamaji
Tangu kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji kuna mambo mengi ya kujivunia ambayo yamefanywa na kamandi hii kwa ajili ya taifa letu;
a. Ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi pande zote za bahari ya Hindi na bandari zote nchini umeimarika. Hii imeifanya nchi yetu kutoingiliwa na adui kirahisi na imekuwa na mipaka ya bahari iliyo salama.
b. Kamandi iliweza kushiriki kikamilifu katika vita ya Kagera ambapo ilitoa mchango mkubwa kupitia kwenye ziwa Victoria. Meli vita aina ya Topido Squadron chini ya Meja Joachim Lisakafu walifanikiwa kuangusha ndege mbili za adui zilizokuwa zikivuka ziwa Victoria kuja kushambulia nchini. Baadaye alipandishwa cheo hadi kufikia cheo cha Brigedia Jenerali na kuwa Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji hadi alipostaafu na cheo hicho.
c. Kamandi inashirikiana na Wizara ya Ujenzi katika kutengeneza vivuko mara tu vinapoharibika, na kutoa elimu ya usalama baharini kwa wananchi.
d. Kamandi inashirikiana na wizara ya uvuvi na mifugo katika kupambana na wavuvi haramu katika eneo lote la bahari na maziwa.
e. Kamandi imefanikiwa kupambana na kuzuia uhalifu na uharamia baharini kwa kushirikiana na Majeshi rafiki ya Marekani, Uingereza, China pamoja na Afrika ya Kusini.
f. Mahusiano yetu kimataifa yameongezeka, hii ni kutokana na Jeshi letu la Wanamaji kushiriki kutoa mihadhara katika makongamano ya kimataifa yahusuyo mambo ya Jeshi la wanamaji. Mfano katika mikutano ya Jumuiya za Kikanda kama vile Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
g. Kamandi ya Jeshi la Wanamaji ilishiriki vilivyo katika operesheni ya kumuondoa Kanali Bakari huko Comoro aliyeasi na kujitangazia madaraka ya kuiongoza nchi hiyo.
h. Kamandi inashiriki katika operesheni mbalimbali za uokoaji mara tu ajali inapotokea, mfano ilipotokea kuzama kwa meli ya MV Bukoba mwaka 1996 huko Mwanza, kamandi hii kwa kushirikiana na wapiga mbizi kutoka nchi ya Afrika Kusini ilifanya uokoaji wakati wa ajali hiyo.
Matarajio ya Kamandi
Kamandi ya Wanamaji kama ilivyo kwa Kamandi nyinginezo, inayo malengo iliyojiwekea kwa ajili ya kutimiza wajibu na majukumu yake kama:-
a. Kuendelea kuimarisha ulinzi wa mipaka yote ya bahari na maziwa ili kuendelea kuifanya Tanzania kuwa salama wakati wote.
b. Itaendelea kushirikiana na majeshi rafiki kuhakikisha kuwa Bahari ya Hindi katika Pwani ya Afrika Mashariki inaendelea kuwa salama.
c. Kamandi itaendelea kutoa mafunzo kwa watendaji wake mara kwa mara iii kwenda na mabadiliko ya sayansi na teknolojia mpya.
d. Kamandi itaendelea kushiriki mazoezi ya ndani na yale ya kimataifa kwa ajili ya kubadilishana uzoefu
Kamandi ya Nchi Kavu
KAMANDI YA JESHI LA NCHI KAVU
Kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu
Kuundwa kwake kumekuja miaka 43 baada ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanzishwa mwaka 1964.
Hii imekuwa ni historia katika kuleta mageuzi ndani ya Jeshi kwa kuliweka katika muundo utakaoleta ufanisi na tija zaidi katika Ulinzi na Usalama wa Taifa. Aidha, tukio hilo la kuanzishwa kwa Kamandi hii ni tukio la kihistoria la maendeleo ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.
Kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kumetokana na dhamira safi ya Viongozi wa Serikali na Makamanda kuona umuhimu wa kuwa na Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ili kusimamia majukumu ya kiutendaji na kiutawala. Kwa sasa Makao Makuu ya Jeshi yamebakia na majukumu ya mipango na uamrishaji pekee.
“Leo ni siku muhimu kwani tunashuhudia mabadiliko ya muundo wa Jeshi letu ambalo sasa litaundwa na Kamandi tatu yaani Kamandi ya Wanamaji, Anga na Nchi Kavu”. Alisema Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 4 Machi 2009, alipokuwa akizindua rasmi Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu mbele ya maafisa, wapiganaji na wananchi.
Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ina kazi ya msingi ya kusimamia utendaji wa kila siku wa Vikosi,Shule na Vyuo vilivyo chini ya Kamandi hiyo. Kamandi pia inaongoza vikosi vyote vya mizinga na vifaru, vikosi vya wahandisi wa medani pamoja na vyuo na shule zinazotoa mafunzo ya Kijeshi.
Muundo wa Kamandi hii unabakia kuwa wa Kimataifa kwa vile umezingatia viwango vyote vya msingi katika kuanzisha Kamandi na kusimamia majukumu yake ya kimkakati na kisera wakati wa utendaji kazi.
Mara baada ya kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tarehe 01 Septemba, 1964 Vikosi vya Nchi Kavu vilianza jukumu la kufundisha wapigania uhuru na hatimae nchi mbalimbali zilikombolewa kutoka kwa serikali dhalimu za kikoloni. Nchi kama Msumbiji, Zimbabwe, Afrika ya Kusini, Angola na Namibia zilinufaika na msaada uliokuwa ukitolewa na JWTZ. Baadaye Jeshi la Nchi Kavu lilipata jukumu la kuendesha na kusimamia Operesheni ‘SAFISHA’ nchini Msumbiji wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 1986 na 1988.
Ulinzi na Usalama wa Tanzania ni jukumu la kila raia, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alihimiza hilo mara kwa mara ambapo Jeshi lilitekeleza sera hiyo kwa kutoa mafunzo ya mgambo na kuyasimamia kikamilifu.
Mafunzo ya mgambo mpaka leo hii yanamuitikio mkubwa wa wananchi kwani hujiandikisha na kufanya mafunzo kwa hiari.
Mafunzo hayo yamebaki kuwa ni sehemu muhimu ya Jeshi la Nchi Kavu hadi Jeshi linapotimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Katika Vita ya Kagera 1978/79 Jeshi la Nchi Kavu lilinufaika kwa kuwajumuisha wanamgambo na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, kwani wote kwa pamoja walisonga mbele kukabiliana na majeshi ya Nduli Iddi Amin kwa kusaidiana na Vikosi vya Ulinzi wa Anga na Wanamaji, hatimae kuikomboa ardhi ya Tanzania na kufanikiwa kuuondoa utawala dhalimu wa Idd Amin nchini Uganda.
Baada ya vita Serikali ya nchi hiyo iliomba baadhi ya Wanajeshi wa Tanzania wabakie na kutoa mafunzo kwa Jeshi la nchi hiyo. Vikosi vya Nchi Kavu pia vimetoa mchango mkubwa wakati wa maafa na katika ulinzi wa amani duniani kwa kushiriki katika operesheni nchini Liberia, Lebanon, Comoro, Sudan katika jimbo la Darfur na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Kihistoria, majukumu na kazi zote za Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ilizonazo sasa, zilikuwa zinatekelezwa chini ya Makao Makuu ya Jeshi. Makao Makuu ya Jeshi kupitia Brigedi na Vikosi ilifanya kazi na kutekeleza majukumu hayo kwa umahiri na ufanisi wa hali ya juu na hatimae wakati ulifika na kuona ipo haja ya kuboresha muundo wa Jeshi letu ndipo Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ikazaliwa.
Wakati tunaadhimisha Jubilee ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tarehe 01 Septemba 2014, Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu tayari imetimiza miaka saba tangu kuanzishwa kwake mnamo tarehe 25 Disemba 2007 kabla ya kuzinduliwa rasmi tarehe 04 Machi 2009 na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu yapo katika Kijiji cha Msangani, Wilaya ya Kibaha katika Mkoa wa Pwani ambapo Mkuu wake wa Kwanza kuiongoza Kamandi alikuwa Luteni Jenerali Wynjones Kisamba(mstaafu), aliyeiongoza kuanzia 2007 hadi 2011 wakati huo akiwa Meja Jenerali.
Meja Jenerali Salim Mustafa Kijuu (mstaafu) aliteuliwa kuiongoza Kamandi hiyo kuanzia 2011 hadi 2016, akiwa ni Kamanda wa Pili tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007. Kuanzia mwaka 2016 hadi 2017 Kamandi hii ilikuwa chini ya uongozi wa Meja Jenerali James Aloyce Mwakibolwa (kwa wakati ule ) ambaye baadae alipandishwa cheo na kuwa Luteni Jenerali, hatua iliyoambatana na kuteuliwa kwake kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania mpaka alipostaafu mwaka 2018.
Kuanzia 2017 hadi tarehe 13 Februari 2018, Kamandi ilikuwa ikiongozwa na Meja Jenerali Sharif Sheikh Othman ambaye kwa sasa anaiongoza Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi iliyopo Mgulani Jijini Dar es Salaam.
Kwa sasa Kamandi hii ipo chini ya Meja Jenerali George Thomas Msongole kuanzia tarehe 14 Februari 2018 akipokea kijiti hicho toka kwa Meja Jenerali Sharif Sheikh Othman.
Majukumu ya Kamandi
Kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu kumerahisisha na kuimarisha kwa kiasi kikubwa utendaji kazi wa Jeshi kwa ujumla. Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu imeweza kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa chini ya uongozi wa Makamanda waliotangulia.
Pamoja na majukumu makubwa yanayotekelezwa na Kamandi hii, pia zipo Shule chini ya kamandi kama vile Shule ya Mafunzo ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Ardhini (Infantria -SMI) ambayo inatoa mafunzo bora kwa Jeshi la Nchi Kavu la Tanzania.
Mafunzo ndio uti wa mgongo katika utendaji kijeshi kwasababu huwajengea maafisa na askari uwezo katika kutekeleza majukumu yao ya msingi, mafunzo yamepewa kipaumbele cha pekee katika Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu.
Licha ya kuwa na majukumu ya usimamizi wa Shule ya Mafunzo ya Jeshi la Ardhini, Kamandi pia inazisimamia Shule nyingine za Mafunzo ya Kijeshi kama vile; Shule ya Mizinga (School of Artillery), Shule ya Mafunzo ya Vifaru (SMV) na Shule ya Uhandisi wa Medani.
Umuhimu na matumizi ya taaluma na mbinu zitolewazo na shule hizi huonekana kwa urahisi na wepesi pale Kamandi inapokuwa imepewa jukumu katika uwanja wa medani. Mafunzo yanayotolewa na shule hizo ni kwa ajili ya kuwaandaa maafisa na askari kwa kuwajengea uwezo wa kufanya kazi na kamandi nyingine wakati wa vita.
Ili Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu iweze kufanyakazi zake kwa ufanisi katika kurahisisha utendaji na utoaji huduma kwa kamandi nzima kuanzia Makao Makuu ya Kamandi hadi kwenye Vikosi na Shule. Matawi matano yameundwa na kukabidhiwa utekelezaji wa majukumu hayo, matawi hayo ni pamoja na Tawi la Utumishi, Tawi la Fedha, Tawi la Oparesheni na Mafunzo, Tawi la Usalama na Utambuzi pamoja na lile la Ununuzi na Ugavi.
Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, imekuwa na majukumu ya Kitaifa na Kimataifa kwa vile kuwaandaa maafisa na askari wanaoshiriki katika ulinzi wa amani nchini Sudan, Congo (DRC) , Lebanon, Afrika ya Kati na Sudan Kusini.
Kwa hapa Tanzania, majukumu ya msingi ya Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ni pamoja na kulinda na kuimarisha usalama wa mipaka ya nchi kwa kushirikiana na Kamandi ya Anga na Kamandi ya Wanamaji.
Kamandi hii hushirikiana na Kamandi nyingine ili kuleta ufanisi na tija katika suala la utendaji kazi na kulifanya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liwe la kisasa zaidi.
Aidha wakati wa Amani, Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu ina wajibu mkubwa wa kuzisaidia mamlaka za kiraia katika kukabiliana na maafa pindi yanapotokea bila kusahau kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa Ulinzi na Usalama wa nchi na mipaka yetu dhidi ya adui yeyote awe kutoka ndani au nje ya mipaka ya Tanzania.
Tangu kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, yapo mafanikio ya kujivunia licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Kamandi hiyo, Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kulinda mipaka ya taifa letu na kuendelea kudumisha amani na utulivu hapa nchini. Kamandi imeweza kukabiliana na maafa yanayojitokeza katika nchi yetu kwa ujasiri wa hali ya juu kama vile mafuriko yaliyotokea katika Mikoa ya Morogoro na Dodoma. Kamandi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuyakabili maafa hayo kwa kujenga daraja la muda katika kijiji cha Gulwe Wilayani Mpwapwa.
Katika kukabiliana na mafuriko hayo Dodoma Kamandi ilijenga makazi ya muda katika kambi nne tofauti ambazo ni Kambi ya Chanzuru, Mazulia na Mkoani Morogoro katika Wilaya ya Kilosa, mafuriko yaliyosababishwa na Mto Mkondoa na kuleta maafa kwa Vijiji vya Mkondoa na Kimamba na kutoa huduma za afya bure na maji safi kwa wakazi walioathirika na mafuriko hayo. Kamandi imeweza kujenga uhusiano mzuri kwa asasi mbalimbali za kiraia katika kuimarisha na kutunza suala la amani na ushirikiano katika taifa. Kwa ujumla, utendaji kazi wa Kamandi hii unaimarika siku hadi siku.
Kamandi ya Anga
KAMANDI YA JESHI LA ANGA
Historia ya Kamandi ya Jeshi la Anga.
Kamandi ya Jeshi la Anga ni moja ya Kamandi muhimu zinazounda Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kiutendaji, kivita na kiutawala. Kamandi ya Jeshi la Anga inayo majukumu ya ziada ya msingi katika kutimiza wajibu wake wa ulinzi wa Anga la Tanzania. Kamandi hiyo inao uzoefu wa kusafirisha maafisa na askari wakati wa amani na dharura, pia husaidia mamlaka za kiraia katika kutimiza wajibu wake na kusafirisha mizigo. Juhudi za awali za kuunda nguvu za Jeshi la Anga ndani ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania zilianza mapema mwaka 1964 pale ambapo kikundi cha maafisa kadhaa walipelekwa nchini Israeli na Ujerumani ya Magharibi wakati huo kusomea urubani. Hata hivyo, wanafunzi waliokwenda kujifunza urubani katika nchi ya Ujerumani ya Magharibi hawakuweza kumaliza mafunzo ya urubani kutokana na kuvunjika kwa uhusiano wa kibalozi baina ya Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi mwaka 1965.
Baada ya jitihada za muda, hatimae kikosi cha usafirishaji wa anga kilianza operesheni mwaka 1969 kikiwa na ndege mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ndege nne aina ya OTTER na zilizosalia za CARRIBOU. Wakati wote wa chimbuko la nguvu za anga shughuli zote za kioperesheni zilizohusu vikosi na vitengo vya ulinzi wa anga viliongozwa na Tawi la Operesheni na Mafunzo (COT) la Makao Makuu ya Jeshi.
Mwaka 1971 kilianzishwa kikosi maalum cha mizinga ya kutungulia ndege kikiongozwa na Kapteni Abdallah, makao yake yakiwepo Mgulani. Maafisa wa mwanzo walipelekwa Pakistan na India kwa mafunzo ya mizinga hiyo. Mwaka huohuo Rais na Amiri Jeshi Mkuu (mstaafu) Mwl. Julius K. Nyerere aliagiza Jeshi lipatiwe ndegevita. Mwaka 1973 timu ya marubani wanafunzi 48 wakiongozwa na Meja JE Luhanga(alistaafu akiwa Meja Jenerali) walihitimu mafunzo yao nchini China na wakaanzisha kikosi cha kwanza cha ndegevita
Maendeleo makubwa yalifanyika katika kipindi cha miaka mitano ambapo idadi ya vikosi na zana za Ulinzi wa Anga viliongezeka. Mwaka 1975 vikosi vya Rada vilianzishwa na kugawiwa kanda za uchunguzi wa Anga, kipindi hichohicho vikosi vya makombora matiifu ya kutungulia ndege (SAM) vilianzishwa katika miji mbalimbali.
Utaratibu wa utendaji kivita na mafunzo wa vikosi vyote vya ulinzi wa anga toka 1974 hadi 1982 ulifanywa na Tawi la Makao Makuu ya Jeshi (MMJ) la Chief of Air Defence (CAD) chini ya Kanali SA Hemedi, ambaye baadae alipandishwa cheo kuwa Brigedia Jenerali.
Majukumu ya Kamandi ya Anga.
a. Kutoa ulinzi wa Anga kwa maeneo muhimu ya kitaifa, kisiasa, kiuchumi na kwa Wananchi,
b. Kutoa ulinzi wa Anga kwa maeneo na vituo muhimu vya kijeshi na mkusanyiko wa Majeshi,
c. Kutoa msaada wa kimapigano kwa operesheni za Majeshi ya Nchi Kavu na Wanamaji,
d. Kutoa msaada kwa mamlaka za kiraia hasa nyakati za maafa ya kitaifa na kusindikiza ndege za viongozi pia hukusanya taarifa za kiusalama,
e. Kuendeleza juhudi za mahusiano ya kijeshi na nchi nyingine kwa njia ya mazoezi ya pamoja.
f. Kushiriki katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.
Makamanda Waliowahi Kuongoza
Kamandi ya Jeshi la Anga, tangu ilipoanzishwa hadi hivi sasa imeongozwa na Makamanda saba wakiwamo wa vyeo mbalimbali ambapo cheo cha chini ni Kanali na cheo cha juu ni Meja Jenerali. Makamanda hao ni pamoja na Brigedia Jenerali Robert Mboma aliyeteuliwa kuongoza Kamandi kuanzia tarehe 15 Februari 1982 hadi tarehe 28 Machi 1985, na baada ya kupandishwa cheo kuwa Meja Jenerali Robert Mboma aliendelea kuongoza kuanzia tarehe 28 Machi 1985 hadi tarehe 28 Machi 1994 alipopandishwa cheo kuwa Jenerali na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi hadi alipostaafu utumishi kwa umri mwaka 2001. Kanali Geofrey Dahal aliteuliwa kuwa Kamanda wa Kamandi ya Jeshi la Anga tarehe 01 Julai 2003 hadi 28 Disemba 2003. Kanali Geofrey Dahal alipandishwa cheo kipya kuwa Brigedia Jenerali tarehe 28 Disemba 2003 na kuteuliwa kuendelea kuongoza Kamandi ya Jeshi la Anga hadi tarehe 25 Aprili 2005 alipofariki kwa ugonjwa. Brigedia Jenerali Charles Makakala aliteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga tarehe 02 Julai 2005 hadi tarehe 16 Octoba 2007 ambapo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Tawi la Mipango Makao Makuu ya Jeshi. Brigedia Festo Ulomi aliteuliwa kuwa Kamanda wa wanaanga kuanzia tarehe 17 Octoba 2007 hadi tarehe 11 Agosti 2009 baada ya kupandishwa cheo kipya kuwa Meja Jenerali aliteuliwa kuendelea kuongoza Kamandi ya Jeshi la Anga tarehe 12 Agosti 2009 hadi tarehe 19 Machi 2012 alipostaafu utumishi Jeshini kwa umri. Brigedia Jenerali Joseph Kapwani aliteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga kuanzia tarehe 20 Machi 2012 hadi 16 Septemba 2012 alipopandishwa cheo kipya kuwa Meja Jenerali na kuteuliwa kuendelea kuongoza Kamandi hiyo hadi tarehe 31 Jan 2016 alipostaafu Jeshini kwa umri. Brigedia Jenerali George Ingram aliteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga kuanzia tarehe 01 Feb 2016 hadi alipopandishwa cheo kipya kuwa Meja Jenerali tarehe 03 Dec 2016 na kuendelea kuongoza Kamandi hiyo hadi tarehe 22 Aug 21 alipostaafu Jeshini kwa umri. Meja Jenerali Shabani Mani aliteuliwa kuwa Kamanda wa Jeshi la Anga kuanzia tarehe 23 Aug 2021 hadi sasa..
Ushiriki wa Kamandi Wakati wa Amani.
Tangu kuanzishwa kwa Kamandi ya Jeshi la Anga, imetimiza wajibu wake kama ilivyokusudiwa kusaidia Taifa. Kamandi ya Jeshi la Anga imeshiriki kwa ukamilifu katika kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii pale inapohitajika kufanya hivyo kupitia kikosi chake cha usafirishaji. Kamandi ilishiriki kubeba chakula cha msaada (mahindi) kutoka Iringa na kusambaza katika mikoa mbalimbali wakati wa janga la njaa mwaka 1974.
Kamandi imesaidia katika uokoaji wa wahanga wa mafuriko katika maeneo mbalimbali nchini kama vile Rufiji mwaka 1984 na 1997, Kilimanjaro na Tanga mwaka 1994, Tabora mwaka 1993, Mbeya na Shinyanga mwaka 2007 na Kilosa mwaka 2010.
Kutokana na uzoefu mkubwa Kamandi ya Jeshi la Wanaanga imekuwa ikishiriki kikamilifu katika mazoezi ya kikanda yanayolenga kuimarisha uwezo wa Jeshi katika kufanya uokoaji wakati wa majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi. Mazoezi ya kikanda ambayo Kamandi ya Jeshi la Anga imekuwa ikishiriki ni pamoja na mazoezi yanayoendeshwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC). Tanzania imekuwa ikishirikiana na Afrika ya Kusini, Zimbabwe, Zambia, Malawi, Namibia, Angola na Swaziland pamoja na nchi mbalimbali duniani.
Kamandi ya Jeshi la Anga imeshiriki katika harakati za uokoaji (search and rescue) mfano katika kuopoa miili iliyotokana na ajali ya ndege ya Yemen visiwani Comoro ambayo ilisukumwa na mawimbi hadi kisiwa cha Mafia, ndege na helikopta za Kamandi zilitumika kwenye operesheni hiyo mwaka 2009 kwa mafanikio.
Mara kwa mara Kamandi ya Jeshi la Anga imekuwa mstari wa mbele kusaidia pale inapotakiwa kufanya hivyo. Mwaka 2011, ndege za Kamandi zilitumika kusafirisha vifaa vya msaada kwa wananchi wa Visiwa vya Zanzibar baada ya kutokea maafa ya meli ya abiria ya MV Spider Islander. Pia kamandi ilitumika kusafirisha vifaa kutoka Dar es Salaam kwenda uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kuwaokoa wachimba madini wakati wa ajali ya migodi kujaa maji na kuua wachimbaji madini huko Mererani mwaka 2008.
Mikakati ya Kamandi ya Jeshi la Anga ni kuendelea kuwa hazina ya Taifa katika kufunza marubani wapya, mafundi ndege, na kuwa na mtandao mpana wa kumiliki anga la Tanzania. Upo uzoefu wenye sura mbili; upande mmoja ni kutambua ujuzi na uzoefu wa mafundi na wahandisi wa Kamandi. Kamandi itaendelea kuwa hazina ya uongozi na kuendelea kudumisha nidhamu ya kazi iliyokwisha kuwekwa na Makamanda na wapiganaji waliowahi kufanyakazi katika Kamandi ya Jeshi la Anga kwa miaka mingi ijayo.
JKT
Jeshi la Kujenga Taifa
Historia ya Jeshi la Kujenga Taifa
Miaka 51 iliyopita, yaani tarehe 10 Julai 1963 Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa rasmi kufuatia utekelezaji wa Azimio la Kikao cha Baraza la Mawaziri. Kikao hicho kilifanyika tarehe 19 Aprili, 1963 chini ya uongozi wa Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Tanganyika hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Wazo la kuanzishwa kwa JKT lilitokana na mapendekezo ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU Youth League), Mkutano uliofanyika mkoani Tabora mwaka 1958 ambalo lilitolewa na Katibu Mkuu wa TANU Youth League wakati huo Ndugu Joseph Nyerere, ambaye sasa ni marehemu.
Sheria Iliyoanzisha JKT
Jeshi la Kujenga Taifa lipo kisheria, kwa vile ilipofika mwaka 1964, Bunge lilitunga Sheria ya kuanzishwa kwa JKT na sheria hiyo iliupa nguvu ya kisheria uamuzi wa mwaka 1963 wa Baraza la Mawaziri wa kuanzishwa kwa Jeshi hilo.
Kwa mujibu wa Sheria ile, kujiunga na JKT ilikuwa jambo la kujitolea. Mwaka 1966 sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho na kuanzisha utaratibu wa kujiunga JKT kwa mujibu wa Sheria.
Utaratibu huu uliwahusu vijana waliohitimu vyuo vikuu, vyuo vya elimu ya juu, kidato cha sita na waliomaliza kidato cha nne ambao wamepata mafunzo kwenye vyuo vya taaluma mbalimbali kama vile ualimu, uganga, uuguzi na kadhalika.
Mkurugenzi wa JKT aliwezeshwa kisheria kuwaita vijana hao kujiunga na JKT.Mwezi Julai 1967, kikundi cha kwanza cha vijana wasomi 64 kilijiunga na JKT katika Operesheni Azimio.
Katika kuunga mkono uamuzi wa Serikali kuhusu kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa, viongozi na wasomi wengine waliohitimu zamani waliamua kujiunga na mafunzo ya JKT. Kwa mfano aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais Mheshimiwa Rashid Kawawa, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mheshimiwa Aboud Jumbe, aliyekuwa Spika wa Bunge Chifu Adam Sapi Mkwawa pamoja na baadhi ya Wabunge na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali walijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa mwezi Januari, 1968 na walifanya mafunzo yao katika kambi ya Ruvu iliyoko Mkoa wa Pwani.
Ili kuweka misingi bora na usimamizi bora wa uongozi, Jeshi la Kujenga Taifa lilikuwa ni Jeshi kamili kwahiyo ilipofika mwaka 1975 JKT iliunganishwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na hivyo kuwa sehemu kamili ya JWTZ.
Kuanzia wakati ule Maafisa na Askari wa JKT wakawa ni wanajeshi wa JWTZ na kutambulika kwa vyeo vya JWTZ. Kabla ya hapo JKT ilikuwa na vyeo vyake vilivyokuwa tofauti na vyeo vya JWTZ. Jeshi la Kujenga Taifa liliendelea na majukumu yake ya kutoa mafunzo kwa vijana wa kujitolea kwa mujibu wa sheria. Hata hivyo, mambo mawili ya msingi yalisisitizwa au kuongezwa katika majukumu ya JKT, kwanza JKT kuwa Divisheni ya uzalishaji ya JWTZ yenye dhamana ya kulipatia Jeshi mahitaji yake ya chakula, mavazi na mengineyo. Pili JKT ndipo mahali pa kutolea mafunzo ya awali ya kijeshi na kwamba JWTZ litaendelea kuajiri kutoka wahitimu wa JKT.
Katika dhamira ya kutimiza wajibu wa kwanza kwa ufanisi mwaka 1982 Shirika la Uzalishaji Mali la JKT (SUMA JKT) liliundwa. Shabaha kuu ilikuwa ni kuwa na chombo madhubuti cha kupanga, kusimamia, kuratibu na kutekeleza majukumu ya uzalishaji mali na kiuchumi katika JKT kazi ambayo shirika linaendelea kuifanya hadi sasa.
Kwa upande wa mafunzo kwa vijana, kwa mfano, zaidi ya vijana 305,625 wamepitia JKT na kupatiwa mafunzo ya kijeshi na stadi mbalimbali za maisha katika fani na nyanja mbalimbali. Miaka ya tisini hali ya utoaji wa mafunzo kwa vijana katika JKT iliathirika. Upatikanaji wa huduma na mahitaji kwa ajili ya mafunzo na uwezo wa kuendesha kambi za JKT kwa jumla ukawa mgumu.
Kuyumba kwa uchumi duniani, kulipelekea kupanda sana kwa bei ya mafuta, kuanguka kwa bei za mazao yaliyokuwa yanazalishwa hapa Tanzania na gharama kubwa ya vita dhidi ya majeshi ya Nduli Idi Amin wa Uganda ndivyo vilivyosababisha uchumi wa nchi yetu kutetereka. Hali hii ilipunguza sana uwezo wa Serikali kutimiza majukumu yake ya msingi katika sekta mbalimbali nchini.
Kurejeshwa kwa Mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa sheria
Kurejeshwa kwa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria ilikuwa ni moja ya mambo yaliyopewa kipaumbele cha juu katika awamu ya nne ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Serikali ya awamu ya nne imerudisha mafunzo ya JKT kwa sababu ya nia njema ya kuendelea kujenga uzalendo kwa vijana wa Tanzania. Itakumbukwa kwamba kutokana na hali ngumu ya kiuchumi serikali ilishindwa kumudu kuendesha mafunzo ya JKT kwa mujibu. Mnamo Juni 15, 1994 mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria yalisitishwa kwa muda.
Jeshi la Kujenga Taifa limefanya kazi kubwa na nzuri ya kujenga moyo wa utaifa na uzalendo miongoni mwa vijana waliopitia katika Jeshi hilo. Hapa ni mahali ambapo vijana wa itikadi zote, rangi zote, makabila yote, dini zote hukutana, kuishi pamoja na kufanya mafunzo na kazi kama ndugu wa familia moja.
Hakuna chombo chochote cha malezi ya vijana kilichoizidi JKT katika kazi hiyo, pengine hata ile tabia ya Watanzania wengi kutoulizana makabila yao inatokana na uwepo wa JKT. Vijana wazalendo wa Tanzania wanaopitia JKT huwa wanakutana na vijana mbalimbali kutoka kila kona ya nchi yetu, ndiyo maana hawana muda hata wa kuulizana makabila kwa vile wote hujiona ni wamoja.
Aidha, athari za kusimamishwa kwa mafunzo ya JKT kuliwagusa wengi na ndiyo maana Serikali ya awamu ya nne imerejesha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria. Hatimaye tarehe 26 Machi 2013 mafunzo ya JKT yalianza ikiwa ni pamoja na kutimiza ahadi ya serikali ya kufufua upya mafunzo hayo katika kambi ya Ruvu.
Kama ilivyokuwa mwaka 1964 JKT ilipoanza na mwaka 1968 baada ya mafunzo ya mujibu wa Sheria kuanzishwa viongozi wa kitaifa waliongoza katika kushiriki mafunzo hayo. Mafunzo hayo ya JKT yalianza na kulikuwa na idadi ya wabunge 22 ambao walishiriki na kumaliza mafunzo ya uongozi. Wabunge hao walitawanywa katika kambi mbalimbali kwa ajili ya mafunzo ya muda wa miezi miwili waliyoomba wenyewe kwa ajili ya kupata mafunzo ambayo wanaamini yatawajengea uzalendo zaidi kwa taifa lao.
Wabunge waliofanya mafunzo ya JKT baada ya kurejeshwa
Kambi ya JKT Ruvu wabunge tisa walihitimu akiwemo, Mhe. Mendrad Lutengano Kigola (MB), Mhe. David Ernest Silinde (MB), Mhe. Easter Amos Bulaya (MB), Mhe. Murtaza Mangungu (MB), Mhe. Yusuph Haji Khamis (MB), Mhe. Neema Mgaya Hamis (MB), Mhe. Halima James Mdee (MB), Mhe. Livingstone John Lusinde (MB) na Mhe. Said Mohamed Mtanda (MB).
Aidha, Wabunge watano walihitimu katika kambi ya Bulombora-Kigoma, ambao ni pamoja na Mhe Sabreena Sungura (MB), Mhe Seleman Said Jafo (MB), Mhe Mariam Kasembe (MB), Mhe Mariam Salum Msabaha (MB) na Mhe Yahaya Kasim Issa (MB). Wabunge watano walikuwa katika Kambi ya JKT Mgambo-Tanga, ambapo waliohitimu ni pamoja na Mhe Zitto Z. Kabwe (MB), Mhe Raya Khamis (MB), Mhe Dr. Anthony G. Mbassa, Mhe Idd Azzan (MB) na Mhe Abdallah Hajji Alli (MB). Kambi ya Msange mkoani Tabora nayo ilikuwa na Wabunge watatu ambao ni, Mhe Meshack Mfukwa, Mhe Rita Kabati na Mhe Mwigulu Lameck Nchemba.
Mkuu wa JKT aliopo na waliopita
Meja Jenerali Rajabu Mabele Mkuu wa JKT kuanzia tarehe 19 May 2021 hadi sasa , Brigedia Jenerali Charles Mbuge Mkuu wa JKT kuanzia Sep 2019 hadi alipopandishwa cheo kipya kuwa Meja Jenerali tarehe 02 Jun 2020 na kuendelea kuongoza Kamandi hiyo hadi tarehe 15 May 2021, Meja Jenerali Martin Busungu Mkuu wa JKT kuanzia Feb 2018 hadi Sep 2019, Meja Jenerali Michael Isamuhyo Mkuu wa JKT kuanzia Feb 2016 hadi Jan 2019 , Meja Jenerali Raphael Muhuga Mkuu wa JKT kuanzia Mar 2012 - Jan 2016 ,Luteni Jenerali Samweli Ndomba Mkuu wa JKT Mar 2012 - Sept 2012 , Meja Jenerali Samwel Kitundu Mkuu wa JKT kuanzia Sept 2008- Jan 2012 ,Meja Jenerali Martin Madata Mkuu wa JKT kuanzia Sept 2007- Sept 2008 , Meja Jenerali Abdulrahman Shimbo Mkuu wa JKT kuanzia Juni 2006 - Sept 2007 , Meja Jenerali Davis Mwamunyange Mkuu wa JKT kuanzia Oct 2001 – Juni 2006 , Meja Jenerali Makame Rashidi Mkuu wa JKT kuanzia Jan 1989 - Oct 2001 , Meja Jenerali Nelson Mkisi Mkuu wa JKT kuanzia Jan 1973 - Jan 1989 , ASP Laurence Gama Mkuu wa JKT kuanzia Mei 1970 - Jan 1973 , ASP Robert Kaswende Mkuu wa JKT kuanzia Mei 1967 –Mei 1970 , ASP David Nkulila Mkuu wa JKT kuanzia Julai 1963 - Dec 1967
Kamandi ya MMJ
8Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi
Kuanzishwa kwa Kamandi
Kamandi ya Vikosi chini ya Makao Makuu ya Jeshi ni Kamandi mpya ambayo uanzishwaji wake ulianza rasmi baada ya kikao kilichofanyika chini ya Halmashauri ya Majeshi ya Ulinzi kwa kupitisha uamuzi wa kuanzishwa kwake mwaka 2013.
Kamandi ilianza kama GOC kwa kufuata mtiririko maalum hadi kufikia Kamandi kamili. Tangu Kamandi ianzishwe iliongozwa na Makamanda wafuatao:
Meja Jenerali HV Chema kuanzia tarehe 01 Jul 14 hadi 28 Sep 14
Brigedia Jenerali JK Mrema kuanzia tarehe 06 Jun 11 hadi 30 Jun 14
Brigedia Jenerali DB Mrope kuanzia tarehe 29 Sep 14 hadi 15 Sep 15
Meja Jenerali IS Nassor kuanzia tarehe 16 Sep 15 hadi 18 Feb 16
Brigedia Jenerali DB Mrope kuanzia tarehe 19 Feb 16 hadi 9 Jul 17
Meja Jenerali SS Othman kuanzia tarehe 15 Feb 18 hadi 30 Jun 20.
Brigedia Jenerali RG Mwaisaka kuanzia tarehe 01 Jul 20 hadi 11 Jun 21, baada ya kupandishwa cheo kipya kuwa Meja Jenerali aliteuliwa kuendelea kuongoza Kamandi hiyo tarehe 11 Jun 2021 hadi hivi sasa.
Majukumu ya Kamandi
Kushughulika na utawala na uendeshaji wa vikosi na shule zilizopo chini ya Makao Makuu ya Jeshi
Kuhakikisha maelekezo yanayotolewa na Makao Makuu ya Jeshi yanawafikia walengwa na yanatekelezwa.
Kusimamia mafunzo na utayari kivita wa vikosi ni wa hali ya juu wakati wote
Kuhakikisha zana na vifaa vinakuwa katika hali nzuri kiutendaji
HUDUMA ZA JWTZ
Afya
JWTZ linatoa huduma za afya katika hospitali zake mbalimbali nchini ambazo hutibu wanajeshi na raia bila kubagua. Hospitali hizi zina wataalamu stahili na vifaa vya kisasa ili kukabiliana na magonjwa hata yale ambayo ni sugu. Huduma za afya ni moja ya maeneo ambayo JWTZ linajivunia kwani katika eneo hili watanzania wengi wamehudumiwa katika maeneo tofauti. Huduma za afya ya uzazi na mapambano ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI na nyinginezo zimekuwa zikitolewa kwa wananchi wote.
Malengo ya Jeshi ni kuzidi kujiimarisha katika kutoa huduma za afya kwa watanzania wote. Hili linaenda sambamba na kusomesha madaktari wengi zaidi na kununua vifaa tiba vya kisasa. Matumaini makubwa ya Jeshi ni kuwa, madaktari hawa au hospitali hizi, zitumike kutoa matibabu kwa watanzania wote hasa wakati wa matatizo mbalimbali ikiwemo migomo. Itakumbukwa kuwa, mara kadhaa kunapokuwepo na migomo ya madaktari na Serikali imekuwa ikitumia madaktari wa Jeshi kuokoa maisha ya makumi kwa mamia ya watanzania katika tiba ya dharura. Kwa mfano, tulishuhudia madaktari wa Jeshi wakitoa matibabu katika vitengo vya utabibu vya hospitali ya Muhimbili wakati wa mgomo mwaka 2012. Madaktari hao mabingwa waliopelekwa Muhimbili walikuwa wa fani tofauti ikiwemo upasuaji, magonjwa ya watoto, na hata wataalamu wa magonjwa ya akinamama na magonjwa mengine mbalimbali.
Maendeleo ya huduma za kijamii Jeshini
Uboreshaji wa huduma za Wanajeshi katika kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, kumekuwa na mkazo wa hali ya juu kuhakikisha kuwa huduma bora na za msingi zinapatikana kwa urahisi ili kuwaandaa wanajeshi kuwa tayari wakati wowote kutimiza wajibu kwa Taifa.
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linalo tawi maalum la tiba Jeshini (CMS). Toka kuanzishwa, tawi hilo limekuwa na majukumu mbalimbali kama vile kusimamia utoaji wa huduma za tiba kwa wanajeshi katika viwango stahili. Majukumu mengine ni kusimamia upatikanaji, uhifadhi na ugawaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vyote Jeshini, Kusimamia uendeshaji wa shughuli za baraza la tiba Jeshini, Kusimamia utawala na uendeshaji wa shughuli za afya na tiba Jeshini pamoja na kusimamia utawala na uendeshaji wa shughuli za Chuo cha mafunzo ya fani ya Afya na tiba Jeshini.Tawi la tiba Jeshini linasimamia utawala na uendeshaji wa shughuli zote za mabaraza ya uchunguzi kwa wanajeshi, familia za wanajeshi na wananchi ambao hupata tiba katika hospitali za Jeshi. Tawi la Tiba linalo wajibu wa kuwasiliana na taasisi za uraiani zinazohusika na mambo ya afya kuhusu namna ya uboreshaji na utoaji wa huduma za tiba Jeshini. Tawi la tiba Jeshini linasimamia na kuratibu wanafunzi madaktari wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika hospitali za Jeshi. Aidha, tawi hilo pia linasimamia uandaaji wa makadirio ya matumizi ya fedha kwa ajili ya shughuli za utoaji huduma za tiba Jeshini.
Huduma za tiba kwa Wanajeshi zinatolewa kwa mujibu wa kanuni za kijeshi kwa utaratibu wa kuzingatia kanuni na maadili ya kitaaluma. Lakini utaratibu wa utoaji wa huduma kwa wananchi unaendeshwa kwa wao kuchangia huduma wanazopata kwa mujibu wa mwongozo wa taifa wa uchangiaji huduma ya afya.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imekuwa ikishirikiana na Tawi la Tiba Jeshini katika kuhakikisha kuna vifaa tiba vya kutosha ili kuongeza uwezo wa hospitali za Jeshi hususani katika huduma za upasuaji wa jumla (general surgery), ajali na mifupa (Orthopedics) pamoja na huduma za wajawazito na watoto. Hospitali ya Rufaa ya Jeshi Lugalo ina historia ndefu iliyoanzia mwaka 1955 ambapo ilikuwa chini ya miliki ya Jeshi la Malkia wa Uingereza (KAR) kwa wakati huo ikijulikana kama kituo cha mapokezi (Medical Reception Station-MRS). Kituo hicho kilichokuwa na daktari mmoja na uwezo wa kulaza wagonjwa 30 tu na kipaumbele kilikuwa ni kwa askari wa Jeshi la KAR.
Baada ya Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 kituo hicho cha tiba kilipanuka na kuendelea kutoa huduma kwa wanajeshi wa TR. Kwa mara ya kwanza huduma hiyo ya tiba iliwahusu familia za wanajeshi na wananchi waliokuwa wanaishi jirani na maeneo hayo.
Wakati wa vita vya Kagera mwaka 1978 hadi 1979 hospitali hii ilijulikana kama Lugalo Garrison Hospital, ambayo wakati huo wa vita ilipeleka jopo la wataalam wa afya na tiba katika eneo la vita. Jukumu lao lilikuwa ni pamoja na kutoa huduma za matibabu ya dharura kwa wapiganaji wa JWTZ waliokuwa katika uwanja wa medani na raia wa Tanzania na Uganda waliokuwa wakiishi katika maeneo ya uwanja wa vita.
Ili kutoa huduma bora zaidi ya tiba, vilianzishwa vituo viwili vya tiba, kituo kimoja kiliwekwa mahali ilipo hospitali kuu ya mkoa wa Kagera kwa ajili ya kuwahudumia majeruhi wa vita. Kituo kingine kilikuwa sambamba na wapiganaji na baada ya kufika Kampala kituo cha tiba kiliwekwa katika hospitali kuu ya Mulago.
Baada ya vita kumalizika, hospitali kuu ya jeshi ilipeleka tena timu nyingine ya wataalam wa tiba mjini Kampala katika eneo la Mbuya kuunda haspitali nyingine ambayo ilihusika na utoaji tiba kwa majeruhi waliokuwa wahanga wa vita na wananchi wa kawaida. Wakiwa katika uwanja wa mapambano, timu ya wataalam wa tiba walihusika na utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa mbalimbali na mazishi kwa waliofariki katika uwanja wa vita. Baada ya vita kumalizika wataalam wa tiba kutoka Tanzania walihusika na upimaji wa afya za vijana wa Uganda kabla ya kujiunga na Jeshi jipya la Uganda kuchukuwa nafasi ya Jeshi lililokuwa limesambaratishwa.
Awamu ya kwanza ya ukarabati wa Hospitali ya Rufaa ya Jeshi Lugalo (GMH) ulianza rasmi mwaka 1994 kwa msaada wa serikali ya Ujerumani na kukamilika mwaka 2001. Ukarabati huo ulihusisha majengo na vifaa, Jeshi limefanya ukarabati wa hospitali zake za Kanda za Mwanza, Mbeya, Bububu - Zanzibar, Tabora, Mazao, TMA (Arusha) pamoja na kuboresha huduma za tiba kwa wanajeshi na wananchi wanaotegemea vituo vya Jeshi kwa huduma za afya. Pia upo ujenzi wa jengo la kutengeneza viungo bandia (Orthopedic workshop) unaendelea.
Kufuatia upanuzi wa majengo na kupatiwa vifaa vya kisasa katika hospitali ya Rufaa ya Jeshi Lugalo, hivi sasa imekuwa na uwezo wa kutoa huduma bora zaidi kuliko ilivyokuwa awali. Hii inachangiwa na ongezeko la rasilimali watu katika fani za madaktari bingwa, uchunguzi wa mionzi, huduma za maabara, huduma za ujauzito kwa mama na mtoto (RCH), ambapo kumekuwa na ongezeko la mahudhurio ya wagonjwa wa nje kutoka wagonjwa 2000 hadi 4000 kwa mwaka 2013. Mafanikio mengine ya hospitali ni kupanuka kwa kozi za kiganga zinazotolewa na shule ya kijeshi ya tiba Lugalo ambayo inaendelea kuimarika katika utoaji wa mafunzo ya Afya katika fani mbalimbali na madaraja ya ujuzi wa tiba mbalimbali hadi mganga mkuu msaidizi Assistant Medical Officer (AMO) kufuatia kuboreshwa kwa miundombinu ya shule.
Elimu
ELIMU JESHINI
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lilianzisha shule za sekondari katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuona umuhimu wa kupandisha kiwango cha elimu kwa maafisa na askari wake. Utaratibu ulifanyika kwa kuazima walimu kutoka Wizara ya Elimu kuja jeshini kufundisha elimu ya Sekondari. Shule hizo ni pamoja na Makongo Sekondari, Air Wing Sekondari, Navy Sekondari (zilizopo Dar es Salaam), Kizuka Sekondari(Morogoro), Luhuwiko Sekondari (Ruvuma), Nyuki Sekondari (Zanzibar) na Unyanyembe Sekondari iliyopo mkoani Tabora.
Kwa kutambua umuhimu wa elimu, pia JKT ilianzisha shule za Sekondari ya Jitegemee iliyopo Kambi ya Mgulani pamoja na Sekondari ya Kawawa iliyopo katika kambi ya Mafinga mkoani Iringa.Lengo la kuanzishwa kwa shule hizo, lilikuwa ni kuwaendeleza maafisa , askari na watumishi wa umma na familia zao kielimu. Aidha baadhi ya vikosi vya JWTZ na JKT vilianzisha shule za msingi na awali (Chekechea) ndani ya makambi.
Michezo
MICHEZO JESHINI
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni moja kati ya mihimili mikuu ya taifa hili siyo tu katika maswala ya ulinzi, bali pia katika michezo. Michezo ni chombo muhimu sana katika kuiunganisha jamii. Aidha michezo huweza kuwa kielelezo na utambulisho wa Taifa kwa njia ya kutoa burudani, kujenga na kukomaza afya ya mwili na akili, kujenga nidhamu, kujitangaza kiuwezo na vipaji. Nchi inaposhiriki katika michezo ya kimataifa, michezo hulitangaza Taifa husika nje ya mipaka yake.
Katika historia ya michezo duniani, Wanajeshi walikuwa wakishiriki michezo mbalimbali tangu enzi za himaya ya kirumi. Michezo hiyo iliwajengea kujiamini na kutambuliwa na jamii zao, hivyo kuiondoa ile dhana iliyojengeka kuhusu Wanajeshi kuwa wao wapo kwa ajili ya vita na mambo ya kutumia nguvu bila akili na maarifa.
Baada ya nchi yetu kupata uhuru, Serikali mpya ya Wananchi ilitambua kuwa michezo ni sehemu ya uhai na utashi wa Taifa letu. Serikali iliunda Wizara ya Utamaduni wa Taifa na vijana mwaka 1962 ambayo ilipewa jukumu la kusimamia maendeleo ya michezo ya Nchi. Sambamba na hilo, Makao makuu ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kuundwa upya mwaka 1964 likaunda Kurugenzi ya michezo na utamaduni ili kutekeleza sera mama ya michezo ya nchi.
Kuundwa kwa Kombania ya Michezo
Kufuatia hitajio la ushiriki wa JWTZ katika mashindano ya Kitaifa na Kimataifa mara baada ya Vita vya Kagera (1979) ziliundwa timu za Jeshi za Kundi la Vikosi na Vikosi chini ya MMJ. Aidha, kufuatia michezo ya majeshi wachezaji walioonekana kuwa na viwango vizuri waliteuliwa kuunda timu teule za jeshi na hatimaye Kombania ya Michezo ambayo ilikuwa chini ya MMJ Kombania ya utawala.
Awali kombania ya michezo iliundwa na timu za Mpira wa Kikapu na Pete. Hata hivyo ili kupanua wigo wa ushiriki baada ya mafanikio yaliyopatikana kupitia timu hizo idadi ya timu teule ziliongezeka na kuhusisha michezo ya Mpira wa wavu, miguu, mikono, riadha, ngumi na magongo.
Kuundwa kwa kitivo cha utimamu wa mwili
Uwepo wa Kombania ya michezo kulisababisha hitajio la kuundwa kwa shule ya kijeshi ya mafunzo ya utimamu wa mwili na michezo, (PT and Sports Wing) hii ni kutokana na uhalisia kuwa isingelikuwa rahisi kutenganisha michezo na utimamu wa mwili kwani ni taaluma mbili zinazotegemeana. Azma ya Shule hiyo ambayo mbali na kutoa mafunzo ya Utimamu wa mwili, pia ilitoa mafunzo ya ualimu na uamuzi wa michezo mbalimbali sanjari na kusimamia ushiriki wa timu teule katika mashindano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Madhumuni ya michezo jeshini
a. Kujenga na kuimarisha afya ya mwili na akili na maisha bora kwa maafisa na wapiganaji.
b. Kujenga tabia ya ushirikiano, upendo, undugu na uzalendo miongoni mwa wanajeshi na jamii.
c. Kujenga moyo wa kishujaa, ujasiri, ukakamamvu na kujiamini.
e. Kutoa burudani kwa wananchi / jamii na hivyo kuiepusha jamii na muda wa kutenda mambo potofu.
f. Kutoa burudani, kulitambulisha na kulitangaza Taifa/ Jeshi ndani na nje ya mipaka yake.
g. Kuimarisha mahusiano kati ya Jeshi na Raia jamii kupitia michezo hivyo kuendeleza moto wa jeshi la wananchi kujitangaza kupitia michezo.
h. Kutambua, kukuza na kuendeleza vipaji vya maafisa na wapiganaji kimichezo.
m. Kujenga mahusiano mazuri kati ya Jeshi letu na majeshi mengine ndani na nje ya nchi.
Aina ya Michezo
Kurugenzi ya Utimamu wa mwili, michezo na utamaduni ndiyo yenye jukumu la kuratibu na kusimamia ushiriki wa wanajeshi katika michezo. Aidha, ushiriki wa JWTZ katika michezo umegawanyika katika makundi yafuatayo:-
a. Michezo ya Kimashindano.
Huu ni ushiriki wa wanajeshi katika michezo ya kimashindano Kitaifa na Kimataifa. Hii ni michezo inayohusisha timu au mchezaji mmoja mmoja inayochezwa ndani ya Jeshi, kitaifa au kimataifa ikiendeshwa kimashindano na ikitawaliwa na sheria za kimataifa. Aidha, ushiriki huu pia uhusisha mashindano yanayoandaliwa na mashirikisho ya Michezo ya Majeshi kutokana na Tanzania kuwa mwana chama wa mashirikisho hayo kama vile:-
(1) Michezo ya Majeshi kwa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (Mfano kuanzia tarehe 18 Augosti 2014 hadi 30 Augosti 2014 JWTZ lilikuwa mwenyeji wa michezo hii).
(2) Shirikisho la michezo ya Majeshi ya Kanda ya Kusini Mashariki mwa Afrika (CISM ESALO-East Southern Africa Liaison Office).
(3) Shirikisho la michezo ya Majeshi la Afrika (CISM OSMA-Organization of Sports Military in Africa).
(4) Shirikisho la michezo ya majeshi ya Duniani Confederation of International Sports of Military (CISM). Mfano mwaka 1993 timu kombaini ya JWTZ ya mpira wa miguu ilishiriki katika fainali za Kombe la Dunia la Michezo ya majeshi iliyofanyika Labat- Morroco.
(5) Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA).
Michezo ya kimashindano imegawanyika katika makundi makuu mawili :-
(a) Michezo yenye msingi wa Kijeshi ambayo siyo kuleta ushindani peke yake bali inaongeza ufanisi wa kutekeleza majukumu ya kijeshi na Taifa . Michezo kama kulenga shabaha, kuvuta kamba, Karate na Judo.Michezo ya kimashindano imegawanyika katika makundi makuu mawili :-
(b) Michezo yenye kulitangaza JWTZ nje ya Jeshi na kukuza mahusiano kati ya Jeshi na wananchi. JWTZ huwakilishwa na timu teule zilizofikia viwango vya kitaifa na kimataifa katika michezo hii. Mfano ni timu za mpira wa miguu zinazomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa za Ruvu JKT, Ruvu Shooting, Mgambo Shooting zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Timu za Kipanga FC na Hardrock za Brigedi ya Nyuki zinazoshiriki Ligi Kuu Zanzibar. Pia zipo timu za Mpira wa Mikono, Wavu, Kikapu, Magongo, Mieleka n.k. Timu za Transit Camp, 977 KJ,82 Rangers, 44 KJ na Rhino Rangers zilishawahi kushiriki ligi kuu ya Mpira wa miguu Tanzania.
b. Michezo kwa Wote
Huu ni ushiriki wa wanajeshi wote katika michezo kama sehemu ya kazi za kila siku. Kama alivyowahi kusema Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere alipokuwa anafunga michezo ya majeshi mwaka 1978 kuwa ”Mazoezi ya mwili ni lazima kama kupumua, hivyo vijana wetu na watu wazima wajenge tabia ya kufanya mazoezi ya mwili”.
Michezo hii hufanyika mara moja au mara mbili kwa wiki vikosini kutokana na mwongozo wa MMJ. Michezo hii hulenga katika kustawisha kudumisha utimamu wa mwili na viungo wa wanajeshi wote. Makamanda wa Kamandi,Fomesheni /Shule, Vyuo na Vikosi ndiyo wasimamizi wakuu wa michezo kwa wote.
c. Ngoma na Utamaduni
Huu ni ushiriki wa J WTZ katika ngoma na utamaduni wenye lengo la kuonyesha na kudhihirisha asili ya utaifa wa nchi yetu.
Hivyo, JWTZ lina vikundi mbalimbali vya ngoma na utamaduni pamoja na bendi za muziki katika Kamandi na vikosi kama vile Mwenge Jazz Band, JKT Kimbunga Stereo, Nyuki Jazz Band,Air Jazz Band (Wana Anga Anga) pamoja na TMA les Mwenge (Wana Checheleka)
Viwanda
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limekuwa likijihusisha na shughuli za uzalizashaji mali kupitia viwanda vyake kwa kutumia wataalamu wanajeshi na watumishi wa umma. Jeshi limekuwa likizalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo zana za kilimo, mashine mbalimbali, malighafi zinazotumika katika ujenzi, kupitia viwanda na mashirika yake, kama Shirika la Uzalishaji mali la Jeshi la kujenga taifa (SUMA JKT), Shirika la Mzinga lililopo Mazao Mkoani Morogoro, Mradi wa Nyumbu uliopo Kibaha Pwani, Kiwanda cha kushona kilichopo Ruvu JKT.
Oparesheni endelelevu.
Darfur (UNAMID)
Lebanon (UNIFIL)
DRC (MONUSCO)
Utaratibu wa kujiunga na JWTZ
Uandikishaji
Mtu yeyote ataandikishwa kujiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa sifa zifuatazo: -
Awe raia wa Tanzania
Awe na Elimu ya kidato cha nne na kuendelea na awe amefaulu..
Awe hajaoa/hajaolewa
Awe na umri kuanzia miaka 18 hadi 25
Awe na tabia na mwenendo mzuri
Awe na akili timamu na afya nzuri
Masharti ya Utumishi
Askari atapewa nambari ya utumishi baada ya kufaulu mafunzo ya awali.
Atalitumikia Jeshi kwa kipindi cha mwanzo cha miaka sita, baada ya hapo atafanya kazi kwa mkataba wa miaka miwili miwili kwa kibali cha Mkuu wa Majeshi.
Maafisa
Bodi ya Uteuzi wa Maafisa (Officers Selection Board)
huwafanyia usaili Askari wenye elimu ya kidato cha sita na kuendelea toka Vikosini na Shule za Askari wapya (Recruitment Schools).
Watakaofaulu masailiano hayo hupewa hadhi ya Afisa Mwanafunzi (Officer Cadet), na hupelekwa Chuoni (Tanzania Military Academy) kwa mafunzo ya Uafisa kwa muda wa mwaka mmoja.
Source:https://www.tpdf.mil.tz/







Comments
Post a Comment