UCHAMBUZI WA CHANZO CHA VITA YA URUSI DHIDI YA UKRAINE NA UTAYARI WA NATO KUISAIDIA UKRAINE.
Serikali ya Urusi inatimiza adhima yake ya kuivamia Ukraine kwa Mpango Madhubuti (Operesheni Maalumu) kwa mujibu wa Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin kama alivyouhabarisha ulimwengu siku ya Alhamis tarehe 24 Februari, 2022, Mwalimu (2022).
Katika kipindi hiki cha sintofahamu ambacho Urusi ikakadiriwa kubakiza hatua chache kuufikia Mji Mkuu wa Ukraine (Kyiv), kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya habari na wachambuzi wa masuala ya Kidiplomasia, Rais wa Nchi hiyo Volodymyr Zelensky ameomba nchi za Muungano wa Umoja wa Kujihami Kaskazini mwa Bahari ya Atlantiki (NATO) kumsaidia hata hivyo hakuna mwitikio chanya mpaka sasa, Mwalimu (2022).
Uchambuzi kuhusu chanzo cha vita;
Vita hii inasemekana kuwa ni zao la tishio la mimbali ya kiusalama lililoletwa na NATO dhidi ya Urusi.
Kasi ya tishio hilo ilipata nguvu zaidi punde baada ya tukio la kuvuliwa madaraka aliyekua Rais wa Ukraine, Viktor Yanukovych mwaka 2014, Mwalimu (2022).
Kwa mujibu wa maandiko mbalimbali mathalani, "Congressional Research Service Report ya Oktoba 5, 2021,"
Rais huyo aling'olewa kwa mapinduzi yaliyochochewa na kutakaswa na Nchi za Magharibi baada ya kujishikiza zaid kwa Urusi kwa misaada mbalimbali na kugoma kusaini Mkataba wa Ushirikiano na Soko Huria na Umoja wa Ulaya.
Jambo hilo lilipelekea maandamano ya halaiki kiasi cha kusababisha Mapinduzi yaliyotokea mwaka 2013 yaliyosababisha aliekua Rais wa Nchi hiyo kukimbilia Urusi mwaka 2014. Jambo hilo lilipelekea mgogoro wa kidiplomasia kiasi cha Urusi kuivamia Ukraine na kutwaa kwa mabavu mji wa Crimea ambao unasadikika kukaliwa na watu wengi wenye asili ya Urusi.
Baada ya Crimea kuchukuliwa na Urusi, kumejengeka imani kwamba Urusi imejiimarisha kiusalama na kupunguza tishio la athari za NATO hususani Marekani katika viunga vya Bahari Nyeusi na ile ya Caspian, Mwalimu (2022).
Hata hivyo, Urusi imeendelea kuhofia NATO inavyopambana kutanua wigo wake kuelekea viunga vya Mashariki mwa Ulaya kwa kuongeza ushawishi wa kimkakati hususani katika Nchi za Ukraine, Belarus na Georgia.
Kwa mujibu wa Kremlin, ongezeko hilo la ushawishi la NATO kunaongeza uwezekano wa tishio kubwa la kiusalama kwa Urusi hususani katika viunga vya Mashariki mwa Ukraine ambapo ni mpakani na Urusi kiasi cha kuathiri sana ushawishi wa Urusi katika viunga vya Kusini mwa Caucasus na Ulaya Mashariki.
Uchambuzi wa uvamizi wa kimkakati wa Urusi dhidi ya Ukraine, Mwalimu (2022);
i) Kupunguza viunga vya wa mpaka wa Ukraine. Hii inatokana na dhana ya mimbali ya kijeshi na kijasusi kuhusu ukubwa wa eneo la mpaka na uwezekano wa Nchi kuvamiwa kwa kutizama umbali kutoka katika mipaka ya Nchi kwenda Ikulu ya Nchi hiyo, rejea andiko la Sheehan (1996). 'The Balance of Power: History and Theory.' Dhana hii ndio zao la Ikulu kujengwa katikati ya Nchi kimkakati ili kupunguza uwezekano wa kufikiwa haraka endapo itatokea uvamizi.
ii) Kutwaa na kukalia viunga vya Donetsk na Luhansk kwa kutumia Serikali zinazofanya kazi kwa mwamvuli wa Urusi.
Viunga vya Donetsk na Luhansk, kwa zaid ya miaka 7 Urusi imekuwa ikishawishi viunga hivyo kujitenga kutoka Ukraine ili kuiathiri Ukraine kiuchumi na kuishawishi nayo kuwa upande wa Urusi.
Aidha, mnamo tarehe 22 Feb, 2022 Urusi imefanikisha hilo kwa kubainisha viunga hivyo kama Nchi huru kwa njia ya viunga vilivyojitenga vya Luhansk People’s Republic (LPR) na Donetsk People’s Republic (DPR).
Viunga hivyo kimkakati vinatengeneza eneo la Donbas ambalo kimkakati ni hazina katika uchumi wa Ukraine kutokana na uwepo wa migodi ya makaa ya mawe na viwanda vingi.
Kwa mantiki hiyo, Urusi kuyatwaa maeneo hayo kunaiathiri Ukraine kiuchumi kiasi cha kuifanya ikae katika meza ya mazungumzo au kusalimu amri.
Rejea Wasielewski na Jones (2022:2) katika chapisho la 'Russia’s Possible Invasion of Ukraine' wakielezea kuwa Urusi kutwaa viunga hivyo kutaiathiri Ukraine kiuchumi na kuifanya Urusi ikuze uchumi wake kiasi cha kuitisha dunia.
Aidha, Urusi kukalia viunga hivyo kunaiathiri zaidi Ukraine kwan kunaifanya Urusi kuikaribia Ikulu ya Ukraine Kyiv kutokana na mpaka kupungua.
iii) kuihadaa na kuzuia Ukraine kujiunga na NATO.
Adhima ya Urusi ni kuiathiri Kiuchumi na Kiusalama Ukraine kwa kuizuia kutumia Bahari Nyeusi kwa kutwaa viunga vya Magharibi mwa Mto Dnepr, Odessa na Transdniestria sanjari na viunga vingine vya kimkakati kama Mariupol na Kherso ili kupata maji kwa wakazi wa Crimea wakati Ukraine ikithibitiwa kutumia bahari hiyo, Mwalimu(2022).
Mikakati hiyo ya Urusi adhima yake ni kuiathiri Ukraine ili isalimu amri na kuilazimisha kujimaliza yenyewe kupitia meza ya mazungumzo pale Minsk, Belarus.
Uchambuzi kuhusu uhalali wa NATO (North Atlantic Treaty Organization) Kisheria kuisaidia Ukraine;
Kwa mujibu wa Sheria NATO haina uhalali wa kuingia mstari wa mbele (frontline) kuisaidia Ukraine.
Baadhi ya viongozi wamethibitisha jambo hili mathalani, Rais wa Marekani Joe Biden, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson na Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg punde baada ya Mkutano kwa njia ya video na viongozi wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja huo mnamo tarehe 25 Feb, 2022 na badala yake wamekubaliana kupeleka vikosi na silaha kwenye Nchi za Poland na Latvia ambazo ni Nchi wanachama wa NATO.
Je, kwa nini NATO wameridhia kupeleka vikosi na silaha Poland na Latvia?
Ukirejea dhana ya Collective Defence katika uanzishwaji wa NATO hususani Ibara ya 51 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1945, NATO hairuhusiwi kuingia kulinda usalama wa nchi ambayo si mwanachama pasipo idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (United Nations Security Council-UNSC)
, Mwalimu (2022).
Hii inamaanisha kwamba, NATO ingekua na uhalali pasi na shaka endapo Ukraine ingekuwa ilisaini Mkataba wa kuanzishwa kwa NATO wa tarehe 4 Aprili, 1949 ambapo Ibara za 5 na 6 za Mkataba huo zingekua nguzo kuu kupata msaada wa moja kwa moja na haraka kutoka NATO ili kulinda usalama wa Nchi mwanachama.
Kwa mantiki hiyo NATO inashindwa kupata uhalali wa kuisaidia Ukraine moja kwa moja.
Aidha, sababu nyingine inayoikabili NATO kushindwa kuingia moja kwa moja kuisaidia Ukraine inasababishwa na Ukraine kutokua mwanachama wa NATO, hivyo idhini ya kwenda hatua zaidi inategemea baraka za Umoja wa Mataifa kupiga kura ili kuazimia kuilinda Ukraine kupitia Baraza la Usalama la Umoja huo (UNSC), Mwalimu (2022).
Katika viunga vya Sheria za Kimataifa, majukumu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hutegemea Ibara ya 39, 40, 41, 42 na 43 za Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Kwa mantiki hii, Azimio la Baraza la Usalama linakuwa kikwazo katika kutatua mgogoro huu kutokana na sababu zifuatazo;
i) Nchi iliopo vitani (Urusi) ni mhusika mkuu katika maamuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
ii) Hata kama kura zitapigwa kuazimia bado kura hizo hazitoi mwanya wa msaada kwa Ukraine kulinda usalama wake.
Hii inatokana na sababu kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) linaundwa na wanachama wapatao 15 waliogawanyika katika makundi mawili;
i) Wanachama wa Kudumu watano (5).
(2) Wanachama wa kawaida kumi (10) wanaopatikana kwa mzunguko wa Nchi wanachama na mgawanyo wa Ukanda wa Nchi wanachama.
Mathalani, Kenya ni miongoni mwa Nchi ambazo sio mwanachama wa kudumu inayoiwakilisha Afrika.
Pingamizi la kusaidiwa Ukraine linatokana na dhana ya nguvu ya Kura ya Turufu (VETO Power).
Veto Power ni Kura yenye nguvu ya kufanya maamuzi ya mwisho (substantive resolution) inayopigwa na Mataifa matano yenye uanachama wa kudumu katika maazimio mbalimbali yanayopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).
Mataifa hayo yenye uwezo wa kupiga Kura ya Turufu ni Urusi, Marekani, Uingereza, Ufaransa na China.
Upigaji wa Kura katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa zingatio la Kura ya Turufu;
Ikumbukwe kwamba, Upigaji wa kura za kupitisha Azimio lolote la Umoja wa Mataifa baraka zake hutegemea angalau kura 9 kutoka miongoni mwa wajumbe 15 wa Baraza la hilo la Usalama.
Aidha, kura hizo 9 zilizopigwa kusiwe na Nchi mwanachama wa kudumu aliepiga kura ya Hapana, endapo itatokea hivyo basi Azimio hilo haliwezi kupata uhalali wa kutekelezwa hata kama Azimio hilo litakuwa limepata kura zaidi ya 11 za kuliwezesha kwenda Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).
Uwezekano wa NATO kuisaidia Ukraine moja kwa moja kwa dhana ya Kura ya Turufu unakwama kutokana na Urusi kwa namna yoyote ile haitaweza kupiga kura ya Ndio hivyo Nguvu ya Kura yake inafanya maamuzi yanayozuia Azimio kupita (Substantive resolution).
Jambo hili linaonyesha udhaifu mkubwa wa Baraza hilo la Usalama kwani hizo Nchi zingine wanachama hazina madhara katika maamuzi hivyo zipo kutimiza matakwa wa mataifa hayo mengine makubwa matano.
Baraza la Usalama lilivyo, Ukraine itapona?
Udhaifu huo wa Baraza la Usalama unatengeneza maswali ya Kisheria hususani kanuni za Asili za Haki (Principles of Natural Justice) hususani "Nemo judex in causa sua" inayobainisha kwamba upande hauwezi kushiriki kufanya maamuzi katika jambo ambalo una maslahi nalo, Mwalimu (2022).
Itakumbukwa kwamba, zao la Urusi kuingia vitani ni maslahi kwa Ukraine na hofu ya Nchi hiyo kujiunga NATO kiasi cha Urusi kuhofia kupoteza soko la biashara yake ya gesi Nchini Ukraine na Nchi zingine za Ulaya ikiwemo Ujerumani. Dhana hii ya udhaifu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linajenga hoja ya kuwa kikwazo kwa mataifa mengine duniani nje ya yale matano yenye nguvu, Mwalimu (2022).
Je, vikwazo dhidi ya Urusi kutoka Marekani na Umoja wa Ulaya vitainusuru Ukraine?
Jibu lina ukakasi kidogo maana vikwazo havitaisaidia Ukraine isiadhibiwe na Urusi kwa muda mfupi ambao vita vinapiganwa japo vikwazo hivyo vitaiathiri Urusi kiuchumi baada ya muda mrefu, Mwalimu (2022).
Hata hivyo, tafiti mbalimbali zinabainisha kwamba vikwazo vinashindwa kutimiza adhima ya kuiathiri Nchi vamizi kusitisha mpango wake wenye athari kwa Nchi nyingine.
Rejea andiko la "Can economic sanctions be effective?" Liliandikwa katika ripot ya Shirika la Biashara Dunian (WTO) mwaka 2018 na mwandishi Smeets (2018), ambapo mwandishi anatanabaisha kwamba hoja ya vikwazo vya kiuchumi kuiathiri Nchi vamizi ni dhaifu sana kwani vikwazo hivyo mara nyingi havizuii Nchi huska kufanya uharifu kutokana na athari ndogo sana dhidi yake.
Dhana hii ndio inamchochea Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy kubainisha kwamba vikwazo pekee kwa Urusi havitoshi bali ili kuisaidia Ukraine Nchi washirika zina kila sababu za kufanya jambo kubwa zaidi kuisaidia.
Rejea;
Charap, S, et el., (2017). The Ukraine Crisis and
the Ruinous Contest for Post-Soviet Eurasia Routledge/IISS
Freedman, L. (2019). Ukraine and the Art of Strategy Oxford University Press.
Kofman .M et al., (2017). Lessons from Russia’s Operations in Crimea and Eastern Ukraine-RAND Corporation.
Mwalimu, A. (2022). Vita ya Urusi dhidi ya Ukraine na Ukweli kuhusu NATO.
Sakwa, R. (2016). Frontline Ukraine: Crisis in the Borderlands I.B. Tauris.






Comments
Post a Comment