Dkt Kipilimba Mkurugenzi mpya Usalama wa Taifa.

RAIS John Magufuli amemteua Dkt Modestus Francis Kipilimba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Taarifa ya Ikulu Jijini Dar es Salaam imesema kabla ya uteuzi huo Dkt. Modestus Francis Kipilimba alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Dkt. Kipilimba anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Rashid Othman ambaye amestaafu.
Taarifa hiyo imesema Dkt. Kipilimba ameapishwa leo mchana Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Rais Magufuli amemteua Bw. Robert Msalika kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa.
Kabla ya uteuzi huo Msalika alikuwa Afisa Ubalozi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Bw. George Madafa kuwa Balozi na nchi atakayopangiwa itatajwa baadaye.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Wakurugenzi na Naibu Wakurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa waliopo wanaendelea na nafasi zao.

Comments

News