MAAFISA WA ZAMANI WA UPELELEZI WAHUKUMIWA KIFO.


 Mahakama ya Gambia imewahukumu kifo wanachama watano wa zamani wa idara ya upelelezi kwa mauaji ya mwanaharakati wa kisiasa wakati wa utawala wa dikteta wa zamani Yahya Jammeh.


 Jaji wa Mahakama Kuu Kumba Sillah-Camara Jumatano alitoa hukumu dhidi ya mkuu wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Taifa, Yankuba Badjie, baada ya kumpata na hatia ya kumuua Ebrima Solo Sandeng, mtu muhimu katika chama cha upinzani cha United Democratic Party, mwaka 2016.


 Badjie pia alipatikana na hatia ya kudhuru mwili.

 Kuhusiana


 Aliyekuwa mkuu wa operesheni wa shirika hilo, Sheikh Omar Jeng, pamoja na maafisa wa NIA Babucarr Sallah, Lamin Darboe na Tamba Mansary, walitiwa hatiani kwa mashtaka hayo hayo na kuhukumiwa kifo na mahakama ya Banjul.


 Sandeng alikamatwa wakati wa maandamano ya Aprili 2016 dhidi ya Jammeh.  Alifariki akiwa kizuizini siku mbili baadaye baada ya kupigwa na kuteswa.


 Kifo chake kilichochea vuguvugu la kisiasa ambalo hatimaye lilimuondoa madarakani Jammeh, ambaye alikuwa ametawala taifa hilo dogo la Afrika Magharibi kwa miaka 22.


 Haruna Susso, afisa mwingine wa NIA, na Lamin Sanyang, nesi, hawakupatikana na hatia ya mauaji au kudhuru mwili.


 Naibu mkurugenzi wa zamani wa shirika la kijasusi, Louie Richard Leese Gomez, pia alikuwa ameshtakiwa lakini amefariki dunia.


 Afisa mwingine, Yusupha Jammeh, alikuwa ameshtakiwa lakini baadaye akaachiliwa huru.


 'Haki inaendelea'


 "Haki inawafikia wafuasi wa Yahya Jammeh nchini Gambia na duniani kote na tunatumai kuwa hivi karibuni itamfikia Yahya Jammeh mwenyewe," alisema Reed Brody, wakili wa Tume ya Kimataifa ya Wanasheria ambaye anafanya kazi na wahasiriwa wa Jammeh.


 Kesi hiyo, iliyoanza mwaka wa 2017, ilikuwa kesi pekee inayoendelea nchini inayohusishwa na uhalifu uliofanywa chini ya utawala wa kikatili wa Jammeh.


 Hapo awali, Yankuba Touray alihukumiwa nchini Gambia kwa mauaji ya 1995 ya waziri wa fedha Koro Ceesay.  Alihukumiwa Julai 2021 na kuhukumiwa kifo, lakini amekata rufaa.


 Mshirika mwingine wa zamani wa Jammeh, Bai Lowe, alifikishwa mahakamani mwezi Aprili nchini Ujerumani, akituhumiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu, mauaji na jaribio la mauaji.


 Waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Ousman Sonko, amekuwa akichunguzwa nchini Uswizi tangu 2017, wakati Michael Sang Correa, anayedaiwa kuwa mshambuliaji, alishtakiwa mnamo Juni 2020 nchini Merika.


 Jammeh amekuwa akishutumiwa kwa uhalifu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ubakaji, matumizi ya vikosi vya mauaji, na kuamuru kupotea kwa maadui wa kisiasa.  Mwezi Mei, mamlaka ya Gambia iliahidi kumfungulia mashitaka.


 Serikali pia ilikubali mapendekezo ya tume ya ukweli ya kuwafungulia mashtaka zaidi ya watu 200 kwa uhalifu uliofanywa chini ya utawala wa rais huyo wa zamani.


 Jammeh mwenyewe bado yuko uhamishoni nchini Equatorial Guinea, ambako alikimbilia mapema 2017 kufuatia kushindwa kwake katika uchaguzi wa Desemba 2016 na Rais Adama Barrow.


 Chanzo: NTV Kenya

Comments

News