Mapinduzi makubwa ya sanaa yahitajika

MWAKA 2017 pengine ni mwaka wa mapinduzi makubwa katika tasnia ya filamu pamoja na muziki. Tunasema hivyo kwa kuwa wengi wa wasanii wakubwa waliohojiwa na vyombo vya habari wamesema kwamba wana vitu vikali watanzania wavisubiri.
Wamesema hayo huku pia kukiwapo na mnong’ono kwamba muziki na filamu unatajirisha watu wengine lakini wasanii hao wapo chini.
Lakini wapo pia wanaosema kwamba tasnia ya filamu inadumaa, hali ambayo inahitaji kuangaliwa tena kwa makini. Kutokana na kuwapo kwa mazingira mazuri ya burudani, mwaka huu ni tarajio letu kwamba kauli zilizotolewa na wakali wa muziki na pia filamu ni dira katika ustawi wa zana hizo mbili za burudani.
Tunachotaka kuwasihi wale wanaoanza na wale wanaoendelea kujipanga vyema, kutambua mazingira na kuibuka katika mstari sahihi wa biashara katika burudani bila kuvunja maadui ili kuleta zogo.
Uletaji zogo ambao tunauzungumzia hapa sio ule wa kutengeneza mistari inayochana au sinema zinazotia wazimu bali mipangilio iliyobora kimenejimenti na kuhakikisha kwamba sanaa hizo zinakwenda halali kulinda maslahi yao na taifa.
Ulindaji huku wa maslahi yao na taifa ni kule kufuata taratibu za burudani kitaifa na kimataifa na kuhakikisha kwamba wanalitambua soko na kulitumia vilivyo.
Kwa misingi hiyo tunasema wasanii wote maana yake wale wanaoonesha,wanaotengeneza na hata wale wanaobuni wanatakiwa kuhakikisha kwamba wanawekea hati miliki kazi zao na pia kutumia mwanya wa kuwapo kwa miundombinu rafiki ya kusafirisha kazi zao kimawasiliano kuuza bidhaa zao.
Tunatarajia toka mwaka jana maprojuza wa muziki na hata wale wa filamu wamejipanga kuonesha makali yao na kutengeneza kitu kitakachouza Tanzania huku masuala ya gere za kuharibiana yakiachwa mwaka uliopita, yaani mwaka 2016.
Kutokana na kuamini kwetu huko tunapenda kuamini kwamba sheria zilizopo na juhudi za Waziri anayesimamia sanaa nchini, wanamuziki, wasanii wa filamu pamoja na washirika wao watakuwa katika nafasi nzuri ya kupima na kutumia utaalamu wao kuuza, kujiuza na kununulika katika soko la burudani nchini na nje ya nchi.
Aidha ni matumaini yetu kwamba wadau hawa hawatasita kumpa ushirikiano wa karibu Waziri wa Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo Nape Nnauye kuhakikisha kwamba wanafanikisha tasnia ya burudani na kupata jasho halali la kazi yao.
Tunazungumzia hivyo kwa kuwa bila tafakari kuna baadhi ya wasanii wameanza figisufigisu na wizara hiyo, ambapo sisi tunaona kwamba kitendo hicho ni cha kuvunjiana heshima, hakifai .
Tangu aingie katika wizara hiyo Waziri Nape amekuwa mtu wa karibu kushughulikia maslahi ya watoa burudani hivyo ni vyema wasanii na yeye wakashikamana katika utendaji kwa lengo la kuifikisha sanaa ya Tanzania katika kiwango kingine cha juu zaidi.
Ni wito wetu kwa wasanii wawe wa filamu au muziki, wawe wa majukwaani au wachonga vinyago watafanya mapinduzi makubwa katika fani hii ili waweze kuneemeka.

Comments

News