Ligi Kuu yafikia patamu

BAADA ya mabingwa watetezi Yanga kuifunga Majimaji bao 1-0 na Simba kutoka suluhu na Mtibwa Sugar, matokeo hayo yamefanya mbio za ubingwa kunoga. Simba ambao wanaongoza Ligi Kuu kwa tofauti ya pointi mbili, watakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha wanashinda michezo yake ili wapinzani wao Yanga wasiwapite.
Ligi Kuu ya Tanzania Bara itaendelea Januari 28 baada ya kupisha mechi za mashindano ya Kombe la Shirikisho (FA) ambayo yanaanza leo.
Simba katika michezo mitano kuanzia Januari 28 hadi Machi za Ligi Kuu, imecheza mechi nne nyumbani na mmoja ugenini sawa na Yanga na ndio michezo ambayo inaweza kuamua mbio za ubingwa.
Pia timu za Mtibwa Sugar, Azam FC na Kagera Sugar ambazo zote zina pointi 31 zinaweza kuwepo kwenye mbio za kuwania ubingwa, endepo zitafanya vizuri katika michezo iliyobaki.
Hali inaonekana kuwa si nzuri kwa JKT Ruvu ambayo inashika mkia ikiwa na pointi 15 baada ya kushuka dimbani mara 19, lakini kocha wake Bakari Shime alisema anapigana kuhakikisha wanabaki kwenye Ligi Kuu.
Pia Majimaji na Toto African ambazo zina pointi 17 zipo kwenye mstari wa kushuka daraja, endapo hazitabadilika katika mwenendo wake.
Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea Januari 28 kwa michezo sita kuchezwa, ambapo timu ndugu za Kagera Sugar na Mtibwa Sugar watakuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Mbao watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja CCM Kirumba na Ndanda FC wataialika Majimaji kwenye Uwanja wa Nangwanda, Mtwara. Pia JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Stand United, Tanzania Prisons watacheza na Mbeya City Uwanja wa Sokoine na Yanga itaialika Mwadui kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Comments

News