Tetemeko la ardhi laua 73 Italia


Watu 73 wamekufa na wengine 150 hawajulikani walipo baada ya tetemeko la ardhi lenye kipimo cha Richter 6.2 kulikumba eneo la katikati ya Italia leo alfajiri.
Ripoti zimesema wengi wa waliokufa walikuwa mji wa Accumoli karibu na kitovu cha tetemeko umbali mdogo tu kutoka eneo la Amatrice ambalo sehemu kubwa imeharibiwa vibaya.
Kwa mujibu wa ripoti nyumba karibu zote zimeanguka katika kijiji cha Pescara del Tronto na idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka.
Tetemeko hilo limepiga saa 9.36 alfajiri kwa saa za Italia umbali wa kilometa 100 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Rome.
Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi amewapongeza maafisa wa ulinzi wa raia na wa kujitolea waliowahi eneo la maafa katikati ya usiku na wakatumia mikono kuchimbua vifusi vya nyumba zilizoanguka kuwatafuta watu walionusurika.
Ripoti zimesema tetemeko hilo ambalo limeharibu vibaya miji na vijiji viliyopo maeneo ya milima vya Amatrice, Accumoli, Arquata del Tronto na Pescara del Tronto lilikuwa na nguvu kiasi kwamba lilitikisa kwa sekunde 20 katikati ya jiji la Rome na kuhisiwa hadi nchini Croatia.
Pia tetemeko hilo lilihisiwa katika mji wa Bologna uliopo Kaskazini hadi Naples uliopo Kusini. Aidha ripoti hizo zimesema matetemeko madogo madogo 80 yalihisiwa baada ya tetemeko hilo kubwa.

Comments

News