Spika Ndugai aungwe mkono kurejesha maridhiano bungeni
KWA muda mrefu hali ya uelewano baina ya wabunge wa kambi ya upinzani na wa chama tawala, imekuwa tete kiasi cha kusababisha mijadala muhimu inayogusa maslahi ya Watanzania kutojadiliwa vyema kama ilivyokusudiwa.
Hali hiyo, inatokana na ukweli kwamba, pande hizo mbili zimekuwa zikisuguana kila mmoja akitaka hoja yake ipewe kipaumbele, lakini pia suala la kutofuatwa taratibu na kanuni za chombo hicho.
Kumekuwa na vurugu za mara kwa mara, kauli za kejeli, vijembe na wakati mwingine matusi zimekuwa zikitawala ndani ya bunge hilo, kiasi cha kuamsha hasira na kusababisha vikao vya chombo hicho kusitishwa mara kwa mara.
Hali hiyo imekuwa ikiathiri utendaji wa bunge hilo lililo na wabunge zaidi ya 300 wengi wao wakiwa wamechaguliwa na wananchi kwa ajili ya kuwawakilisha ndani ya chombo hicho. Katika mkutano wa tatu wa Bunge la 11 uliomalizika hivi karibuni uliokuwa maalumu kwa ajili ya kujadili na kupitisha bajeti ya serikali, mvutano huo ulionekana dhahiri kiasi cha upande wa upinzani kususia vikao vya bunge hilo kwa kipindi cha mwezi mmoja.
Kususia huko, kuliathiri shughuli hizo za Bunge kwa kuwa hoja nyingi za bajeti zilizowasilishwa ndani ya chombo hicho zilihitaji ushiriki wa wabunge wa pande zote mbili kwa maana ya maoni, michango na mijadala ili kuboresha bajeti iliyopangwa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Hoja kubwa ya upande wa upinzani ni kutomkubali Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kwa madai kuwa amekuwa hafuati kanuni za Bunge na ameonesha kupendelea upande mmoja.
Pamoja na kuwasilisha malalamiko yao kwa mujibu wa taratibu bado bunge hilo lilimalizika bila kuwapo na ushiriki wa upande wa upinzani, hali ambayo haikumfurahisha Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye kwa kipindi cha takribani miezi miwili alikuwa India kwa matibabu.
Spika Ndugai, mara aliporejea nchini mkakati aliojiwekea ni kurejesha maridhiano ndani ya chombo hicho ambayo kwa mujibu wake, hali ilikuwa mbaya kiasi cha wabunge wa pande hizo kutosalimiana wala kualikana katika shughuli za kijamii.
Wakati umefika kiongozi huyo kuungwa mkono na wananchi na wadau wa masuala ya siasa, lakini pia wabunge wanatakiwa kuhakikisha bunge hilo, linakuwa na uwakilishi wa pande zote kwa maridhiano yatakayosaidia nchi kupiga hatua katika suala zima la maendeleo.
Wabunge ni wawakilishi wa wananchi bila kujali itikadi zao, hivyo wanapaswa kuwa kitu kimoja wanapokutana na kuzungumzia mustakabali wa nchi na maslahi mapana ya wananchi wanaowawakilisha.
Maridhiano hayo ambayo kwa mujibu wa Ndugai yanaweza kushirikisha maspika wastaafu, yaungwe mkono na pande zote mbili kwa kuweka tofauti zao pembeni na kuhakikisha wanaanika chanzo kikubwa cha mgogoro unoendelea ndani ya chombo hicho ili kupatiwa ufumbuzi.
Hakuna asiyefahamu kuwa kazi kubwa ya viongozi wa upinzani ni kutoa hamasa na msukumo kwa chama tawala katika suala zima la maendeleo, hivyo endapo kuna mvurugano baina ya pande hizo mbili ni vigumu serikali kuzijua changamoto zinazoikabili ili izifanyie kazi.
Ni matarajio ya Watanzania kuona chombo hiki kinarejesha nidhamu ya wabunge kwa kuwajengea misingi ya kuvumiliana, kupeana nafasi katika kuwasilisha hoja zao bila kujali upande wowote, lakini kubwa zaidi ni kushiriki kikamilifu katika shughuli za Bunge bila kupeana fursa ya kuvurugana au kuvunjiana heshima.
Mkutano wa nne unatarajiwa kuanza rasmi mwezi ujao, ni wazi kuwa jitihada hizo za Spika Ndugai zitazaa matunda, na Watanzania watashuhudia chombo hicho kikijiendesha kwa misingi na kanuni zake huku maridhiano yakipewa kipaumbele.






Comments
Post a Comment