Kukosekana uzalendo kunavyoua soka Arusha

Kukosekana uzalendo kunavyoua soka Arusha.

UNAPOZUNGUMZIA soka la Arusha jinsi lilivyokuwa la ushindani miaka ya nyuma huwezi kuamini kama ndio limepotea.
Kufifia na hatimaye kupotea kabisa kwa soka hilo mkoani Arusha kunatokana kwa kiasi kikubwa na watu wachache kujifanya ndio wanajua zaidi kuliko wengine. Ndani mwake kuna viongozi, wadau wa soka waliokosa ushirikiano na uzalendo kuamua kususa katika kusaidia na kuwa wamoja na badala yake wanaangalia maslahi yao na kusahau majukumu yao.
Arusha ni mkoa wenye sifa za kipekee, lakini kwa hali ya sasa hauwezi tena kuzungumzia soka kwani umepotea kwa kiasi kikubwa na hii ni kutokana na timu zilizokuwa zikifanya vizuri miaka ya nyuma kama vile AFC kushindwa kurudisha muonekano wake. Ndivyo wadau mbalimbali wa soka jijini hapa kwa nyakati tofauti wamekuwa na hofu juu ya mwenendo mzima wa mkoa wao, hasa juu ya kusuasua katika harakati za kuwa na angalau timu moja iliyo katika Ligi Kuu.
Wadau wa soka wanasemaje?
Denis Shemtoe mmoja wa wadau wakubwa wa soka mkoani Arusha ambaye pia aliwahi kuwa katibu mwenezi wa timu kongwe ya AFC miaka ya 1994, anasema hivi sasa Arusha iliyokuwa zamani si hii, kwani imepoteza mwelekeo na hii ni kutokana na viongozi waliopo kukosa dhamira ya kweli kusaidia mpira uendelee.
“Mkoa wa Arusha kwa ujumla umeshindwa kukidhi na kuendana na kasi ya mabadiliko katika kuhakikisha kunakuwa na hamasa kwenye michezo, hali iliyofanya tuwe nyuma kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma, tumepitwa na Mbeya na Tanga ambazo kwa kweli zimeonesha nia,” anasema Shemtoe.
Anasema, hivi sasa wananchi wamekatishwa tamaa kabisa wakati walikuwa wapenzi wakubwa wa soka kwani wameshindwa kuona juhudi zikifanyika kwa viongozi wa vyama vya mpira kuanzia wilayani hadi mkoa, jambo lililowafanya wakazi mbalimbali wa Arusha kuona Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kama sehemu ya kupumzikia.
“Ukiangalia moja ya timu ambazo zilikuwa tishio na mpaka leo tunavyozungumza imebaki historia tu, tulikuwa na timu ya AFC ambayo ilipoteza kabisa mwelekeo na hiyo ilitokana na kukosekana kwa ushirikiano baina ya viongozi wa klabu na vyama vya soka vya wilaya na mkoa, vivyo hivyo na kwa timu zingine ushirikiano umekuwa hafifu. Timu zinapambana kushinda kwa juhudi zao binafsi hakuna hata kiongozi wa chama cha mpira anayewaunga mkono hilo ni tatizo”.
Aidha, anasema kuwa hivi sasa Arusha kwa upande wa soka inakabiliwa na uchaguzi mkuu wa viongozi wa chama cha mpira (ARFA) utakaofanyika Oktoba mwaka huu na kuwataka wapiga kura kuchagua viongozi watakaoleta maendeleo ya soka. “Nadhani sasa labda tutegemee safu mpya itakayoingia madarakani iwe na moyo wa dhati kubadilisha hali hii viongozi watakaojua jinsi wanaweza kurudisha hamasa na Arusha ikafanya vizuri zaidi kwa miaka miwili ijayo,” aliongeza.
Naye Bahati Lumato ambaye aliwahi kuchezea timu mbalimbali ikiwemo Lipuli Kids ya Iringa miaka ya 1970, anasema wapenzi wa soka wamekata tamaa kutokana na kukosekana kwa hamasa baina ya viongozi waliopo tofauti na miaka ya nyuma ambayo kweli ilikuwa Arusha mkoa ulikuwa ukisifika kwa timu nzuri.
“Ifike mahali viongozi wanowania kuongoza katika soka wajaribu kurudi na kuangalia ni mbinu gani zilitumika na zikasaidia kuboresha watafute hata wachezaji wa zamani wapate ushauri wanaweza kusaidia kwa namna moja ama nyingine, vile vile viongozi wabuni mbinu bora ikiwamo kuandaa mashindano mbalimbali ili kurudisha imani kwa wakazi na wapenzi wa soka jijini hapa.”
Kuelekea uchaguzi mkuu wa chama cha soka mkoa Arusha, Lumato anasema kinachotakiwa watu wabadilike wachague viongozi walio na nia na uchungu ambao wataamua kuepeleka mpira wa Arusha mahali sahihi. Hali ilivyo sasa Mkoa huu ulio katika ukanda wa Kaskazini uliokuwa na historia ya kufanya vizuri katika kusakata kandanda miaka ya nyuma zikiwemo timu ya Ndovu FC, AFC Arusha, Ushirika ya Moshi lakini kwa sasa kuna timu nne zilizo katika daraja la pili, ambazo ni JKT Oljoro, Arusha FC, Madini SC na Pepsi FC.
Timu za JKT Oljoro na AFC zilikuwa zikifanya vizuri katika mashindano ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara miaka ya nyuma kabla ya kupotea kabisa katika ulimwengu wa soka na hatimaye kubaki kushuka katika ligi za chini tofauti na matarajio kwa jinsi zilivyokuwa na uwezo. Maafande wa JKT Oljoro waliokuwa tishio katika soka la Tanzania walipanda Ligi kwa mara ya kwanza msimu wa mwaka 2012/2013 na 2013/2014.
Hali haikuwaendea vizuri maafande hao kwani waliboronga na kushuka kutoka Ligi Kuu hadi ligi daraja la kwanza msimu wa 2014/2015 kwa kukutwa na kosa la kupanga matokeo kwenye ligi daraja la kwanza dhidi ya Polisi Tabora kwenye mchezo wa mwisho pale Oljoro walipokubali kichapo cha mabao 7-0.
Kutokana na hali hiyo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndipo lilipoamua kuchukua hatua kali kwa timu zote zilizohusika katika madai ya rushwa hali iliyowafanya wapambane bila mafanikio yoyote kwani hata msimu wa mwaka 2014/15 walichemsha na kuziacha timu za Toto Africans ya Mwanza na Mwadui FC ya mkoani Shinyanga zikipanda Ligi Kuu. Pamoja na kupoteza matumaini kwa msimu huo, Oljoro haikukata tamaa bali iliendeleza dhamira yake ya nini kifanyike katika kuhakikisha inarejea tena kushiriki ligi kuu soka Tanzania bara.
Walipochemsha Oljoro Baada ya kufanya vizuri kwa nyakati tofauti hasa katika harakati zake za kushiriki ligi daraja la kwanza msimu wa mwaka 2015/2016 kwa kuhakikisha inarudi kwa kishindo Ligi Kuu, lakini mambo hayakwenda vilivyo baada ya kukumbwa na sakata la upangaji wa matokeo katika mchezo wa mwisho wa FDL hali iliyopelekea kukumbwa na adhabu ya kushushwa daraja la pili (SDL) baada ya kamati ya nidhamu kutolea maamuzi ya shauri ya upangaji wa matokeo wa kundi ‘C’ FDL.
Katika hukumu hiyo, Klabu za Geita Gold, JKT Oljoro na Polisi Tabora zikakutwa na balaa la upangaji wa matokeo na kupewa adhabu ya kushushwa daraja mpaka ligi daraja la pili (SDL) msimu ujao wakati JKT Kanembwa FC ikishushwa daraja mpaka kwenye ngazi ya ligi ya mkoa (RCL) na kuua ndoto zote.

Comments

News