Koffi Olomide awe funzo kwa wengine
HAYA NDIYO MAISHA.
UNAPOTAJA jina la Mwanamuziki wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo(DRC), Koffi Olomide, sidhani kama kuna mtu asiyemfahamu hasa kwa kilichotokea siku chache zilizopita na kumuingiza matatani na vyombo vya sheria.
Koffi amehukumiwa miezi 18 jela, kwa kitendo alichofanya alipotua nchini Kenya kwa ajili ya onesho lake la muziki lakini akaruhusu mihemuko na hasira imtawale na kujikuta akimpiga mcheza shoo wake. Tukio hilo limeamsha hisia kwa watu katika nchi mbalimbali, ambako walibahatika kuona video ya tukio hilo iliyosambaa katika mitandao ya kijamii.
Haijulikani hasa ni jambo gani lilitokea pale katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kenya, hadi nguli huyo wa muziki wa Kikongo kuamua kutembeza mateke kwa mwanadada huyo, huku akishuhudiwa na wanamuziki wengine waliofuatana na Koffi hadi askari wa Kenya wakaingilia kati kumnusuru dada huyo asiendelee kupigwa.
Kwa kweli ni tukio la kufedhehesha na linatia hasira kuona mwanamuziki huyo akimpiga mcheza shoo wake mateke, kwanza utadhani alikuwa anapigana na mwanamume mwenzake kumbe mwanamke. Kitendo alichofanya Koffi, hakipaswi kuchekewa hata kidogo na kama ndio ulikuwa mtindo wake, basi kifungo chake kiwe fundisho kwake na wote wanaofanya matendo kama hayo.
Mnaweza kujiuliza ni kwa nini nimelizungumzia hili, si kwamba nalizungumzia kwa sababu aliyepigwa ni mwanamke hapana, katika kupiga hakuna jinsia kwa sababu si haki kwa mtu yeyote yule kumpiga mwenzake haijalishi ameudhiwa, amekwazwa au kakosewa kiasi gani.
Tukio la Koffi linaonekana wazi na hasa kwa kuwa ni mtu maarufu, ndio maana lilisambaa kwa haraka na hatua za haraka zikachukuliwa nchini Kenya kwa kumrudisha kwao na DRC nao wakamchukulia hatua haraka ya kumkamata, kumhuku na kumfunga miezi 18 jela.
Yapo matukio mengi ama tunayafahamu ambayo jamii inaamua kuyafumbia macho au hatuyafahamu, ambapo watu wamekuwa wakipigwa na mabosi wao au viongozi wao wa kazi, lakini wanaamua kunyamaza kimya au kuyamaliza kimya kimya tu, jambo ambalo ni hatari kwani kupigwa pigwa kunaweza kuleta madhara makubwa ya kiafya au kifo.
Leo nitazungumzia vitendo vya baadhi ya watu kupiga wafanyakazi wao kwa makosa mbalimbali, kama huamini ndio nakutaarifu wapo watu wanaofanya mambo hayo lakini unakuta kwa kuogopa kuharibu ajira, basi mhusika anakaa kimya tu.
Mfano wako watu wananyanyasika kwenye majumba walipoajiriwa kufanya kazi za ndani, unakuta wananyanyaswa hadi kupigwa lakini wananyamaza kimya tu, ama anasema kwa wenzake au anajikaza tu, jambo ambalo si haki wala si sawa.
Wako wengine wanafanya kazi kwenye maofisi binafsi, wanatembezewa kichapo inapotokea amesababisha hasara au kakosea jambo, lakini mtu anaamua kunyamaza kimya tu akiogopa kupoteza ajira au basi tu anaogopa jamii itamuonaje kwa kumshitaki.
Ndugu yangu hakuna sheria inayoruhusu mtu mmoja kumpiga mtu mwingine, hata kama mtu huyo kakosea kwa kiwango gani. Unapopigwa halafu ukakaa kimya, unampa kibali yule anayekupiga kuendelea kufanya vitendo hivyo vya hatari na iko siku anaweza kusababisha madhara makubwa kwa mtu.
Wito wangu kwa jamii, ikemee tabia na vitendo vya kupigana. Havipaswi kuchekewa, nasisitiza vikemewe na kwa nguvu zote na wale wenye tabia hizo washtakiwe na hatua stahiki zichukuliwe kwa wahusika.






Comments
Post a Comment