Jela miaka 4 kwa kujifanya hakimu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Mbeya imemhukumu kutumikia kifungo cha miaka minne jela Baraka Mwakimu baada ya kupatikana na hatia ya kosa la kujifanya Hakimu wa Mkoa na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Mbeya, Rashidi Chaungu alisema Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na pande zote bila kuacha shaka.
Awali Mwanasheria wa Serikali, Xaveria Makombe aliieleza Mahakama kuwa Septemba 9, mwaka jana mshtakiwa alijifanya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa, Maiko Mteite na kuwarubuni watu mbalimbali fedha kwa minajili ya kuwasaidia masuala mbalimbali ya kisheria.
Mwanasheria huyo aliomba Mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na watu wanaojinufaisha kwa njia za udanganyifu. Mshtakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliiomba Mahakama kumpunguzia adhabu kwa madai kuwa anategemewa na familia yake na ndugu wengine wa karibu.
Sanjari na hayo, Hakimu Chaungu amemhukumu mshtakiwa huyo kutumikia miaka miwili jela kwa kosa la kwanza na miaka minne kwa kosa la pili makosa ambayo Mahakama imeeleza kuwa yatakwenda kwa pamoja huku akimtaka kulipa faini ya Sh 500,000 kama fidia ya mlalamikaji katika shauri hilo na kuionya jamii hususan watu wanaojipatia mali na fedha kwa njia ya udanganyifu.

Comments

News