Hongera Mpango kwa kuwa wazi ulipaji kodi
KATIKA gazeti hili kuna habari inayosema kuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia na kuweka upya malengo yake ya ukusanyaji wa kodi nchini.
Lengo la hatua hiyo ni kuangalia ukusanyaji wa mapato halisi, badala ya kutoa takwimu za mafanikio ya ukusanyaji, ambazo hazina tija. Dk Mpango alisema hayo kwa nyakati tofauti mkoani Kigoma ambako yupo kwenye ziara ya kiserikali.
Anasema bado zipo fedha nyingi, ambazo zinapaswa kukusanywa na mamlaka hiyo na kwamba mamlaka hiyo isiridhike na takwimu za sasa kuwa imevuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa mwaka uliopita na mafanikio makubwa ya kila mwezi.
Alisema bila kuwepo kwa ukusanyaji wa kutosha wa mapato ya ndani, itakuwa vigumu kwa serikali kutekeleza mipango ya kuboresha maisha ya Watanzania na kuifanya Tanzania ijitegemee kwa sehemu kubwa katika matumizi yake na kuondoa mazoea ya kuwa serikali omba omba.
Ili kuhakikisha ukusanyaji mapato unafanikiwa, anasema ni lazima viongozi katika ngazi zote, wapimwe uwezo wao wa uongozi kwa kigezo cha ukusanyaji mapato ya kutosha, na atakayeshindwa kukidhi kigezo hicho, hafai kuwa kiongozi.
Tunampongeza Waziri Mpango kwa kuwa muwazi, kwamba TRA isiridhike kwa mafanikio iliyopata katika mwaka uliopita na ya kila mwezi. Hii si mara ya kwanza kwa waziri huyo kueleza wazi aliyonayo moyoni.
Hivi karibuni, alisema kuwa yeye kama Waziri wa Fedha, asingependa kuwa waziri ombaomba kwa wahisani, ambao alifafanua kuwa baadhi yao wana masharti magumu, ambayo hayatekelezeki kwa maadili ya Watanzania.
Dk Mpango aliyasema hayo alipokutana na makundi ya wafanyabiashara ofisini kwake, ambapo aliwaeleza bayana kwamba njia ya uhakika ya kujinasua kutokana na hali hiyo ni kukusanya kodi ya kutosha. Aliwahakikishia wafanyabiashara hao, kuwa ana dhamira ya dhati ya kufanya kazi kwa kushirikiana na wafanyabiashara wakubwa na wadogo.
Aliwakumbusha kuwa serikali yoyote duniani ni lazima ikusanye kodi, na kwamba wafanyabiashara wanaokwepa au hawataki kulipa kodi kwa mujibu wa sheria, serikali haitawavumilia. Sisi tunaunga pia msimamo huo wa Dk Mpango, kwani serikali zote duniani zinatimiza wajibu wake kwa ufanisi kutokana na kukusanya mapato ya kutosha.
Ni dhahiri kuwa serikali ikikusanya mapato ya kutosha, itaendesha vizuri mipango yake, mfano mpango wa elimu bure. Kwa mfano, hivi sasa serikali inasambaza Sh bilioni 18 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa elimu bure mashuleni na hizo zote zinatokana na makusanyo ya kodi.
Tunaamini kwamba iwapo utamaduni wa kulipa kodi za serikali, utajengeka na kueleweka kwa Watanzania wote, serikali itapiga hatua kubwa na kuwa na uwezo mkubwa wa kuwahudumia wananchi. Kwa hiyo, wafanyakazi, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wa madini na wananchi wote kwa ujumla, tulipe kodi kwa ajili ya maendeleo ya taifa.






Comments
Post a Comment