HAYA NDIYO MAISHA: Hata kama ni sabuni ya roho, uroho huu wa fedha haufai

MSEMO fedha sabuni ya roho haujasemwa kimakosa kwani ni kweli fedha imekuwa kila kitu kwa baadhi ya watu hadi hatua ya kuamua kuuza utu wao.
Fedha imesababisha baadhi ya watu kukosa woga na kufanya mambo ya ajabu, kujidhalilisha na hata kujifedhehesha. Wengine wameweka fedha mbele na wako radhi hata kusaliti watu wengine ama kuwasababishia madhara sababu tu ameahidiwa fedha.
Yapo matukio mengi sana ambayo yanahusisha masuala ya fedha na utu wa mwanadamu lakini leo nimesukumwa kuzungumza kutokana na habari mbili ambazo ziliandikwa na kutangazwa katika vyombo vya habari wiki hii.
Kwanza ni hili la Vyuo Vikuu nchini vilivyopokea fedha za mikopo za wanafunzi ambao hawapo chuoni na kutakiwa kurejesha fedha hizo ndani ya siku saba. Amri ya kurejeshwa fedha hizo ilitolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako baada ya kufanyika uhakiki wa wanafunzi wanufaika wa mikopo kwenye vyuo vya elimu ya juu nchini.
Habari nyingine ni ile ya fedha za Rais John Magufuli kwa ajili ya kugharimia elimu bure nchini kutafunwa kwa njia ya hila zinazofanywa na walimu wakuu za kuongeza idadi ya wanafunzi hewa ili kupata fedha za ziada. Hilo nalo lilibainika baada ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi kumuagiza mkurugenzi na watendaji kufanya uhakiki shule kwa shule ili kubaini wanafunzi hewa, waliowekwa na walimu wakuu.
Matukio haya mawili ni fedheha katika sekta ya elimu kwa kweli, maana najiuliza hapa ni uzembe na kukosa umakini kwa wanaohusika ama ni kutaka kujineemesha kwa kutumia fursa hiyo ya mikopo na fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya wanafunzi na kuboresha elimu nchini?
Mfano suala la mikopo ya wanafunzi, ninaamini kila chuo kina orodha ya wanafunzi wake waliopo na wasiokuwepo, sasa inakuwaje zinakuja fedha halafu wanafunzi wasiokuwepo nao wanapewa, kama sio ujanja ujanja wa baadhi ya watendaji.
Serikali inafanya kila juhudi kutafuta fedha, tena kwa kubana watu wengine kodi na masuala kama hayo ili kuboresha elimu hapa nchini lakini wako baadhi ya watu wanataka kutumia nafasi hiyo tena kujinufaisha.
Wamenishangaza nao hao walimu wakuu waliokosa uzalendo na kuamua kuongeza majina ya wanafunzi ya ziada ili wapate kujinufaisha, ama kweli kuendekeza tamaa kunaweza kusababisha ukapoteza utu wako.
Yaani Watanzania wanabanwa kila kona kulipa kodi, serikali inahangaika kwa kila namna kutafuta fedha ili kuboresha elimu na watoto wetu wasome bure, kumbe wako Watanzania wenzetu wametumbulia macho fedha hizi ili wajinufaishe.
Matumaini yangu mamlaka husika zinawawajibisha inavyostahili wote watakaobainika kwa njia moja au nyingine kufanya ubadhirifu wa aina yoyote katika sekta mbalimbali wakitaka kujinufaisha, kama waliamua kuweka utu wao pembeni bado wanastahili kuwajibishwa vile vile ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo.

Comments

News