Busara itumike suala la Operesheni Ukuta

Busara itumike suala la Operesheni Ukuta.

IKIWA ni siku chache tangu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kitangaze kuzindua ilichoita operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), Serikali, vyombo vya dola, wasomi na baadhi ya wanasiasa, wameonesha wazi kutounga mkono operesheni hiyo.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, operesheni hiyo itakayofanyika kwa mikutano ya hadhara, itakayotanguliwa na maandamano nchi nzima, ina lengo la kupinga huo udikteta na utawala kandamizi.
Hata hivyo, Kamishna wa Polisi, Operesheni na Mafunzo, Nsato Mssanzya katika taarifa yake kwa umma, alipiga marufuku kufanyika kwa operesheni hiyo na kubainisha kuwa jeshi hilo limebaini mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.
Wakati jeshi hilo la Polisi likiendelea kufafanua sababu za kuzuia operesheni hiyo, Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli naye, aliweka wazi kuwa yeyote atakayekaidi agizo la kutoshiriki katika operesheni hiyo kitakachompata hatosahau.
Katika karipio lake dhidi ya operesheni hiyo, Dk Magufuli alifafanua kuwa uongozi wake ni tofauti kwani umelenga katika kuwahakikishia amani Watanzania na yeyote atakayethubutu kuivunja amani hiyo na kuingiza masuala ya vurugu nchini hatovumiliwa.
Aidha Msajili wa Vyama wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, naye alikemea tamko hilo la Chadema na kusisitiza kuwa limejaa lugha ya uchochezi, kashfa, maudhi na lenye kuhamasisha uvunjifu wa amani.
Kiongozi huyo anayesimamia usajili na mienendo ya vyama vya siasa nchini alikikumbusha chama hicho kuzingatia Sheria ya Vyama vya Siasa namba tano ya mwaka 1992 kifungu (2) (c) inayokataza chama cha siasa kutumia au kuhamasisha matumizi ya nguvu au vurugu kama njia ya kufikia malengo yake kisiasa.
Hali hiyo haikuishia kwa vyombo vya utawala pekee, bali hata baadhi ya wasomi walijitokeza na kutoa onyo dhidi ya operesheni hiyo ikiwemo kuvikumbusha vyama vya siasa wajibu wao wa kulinda misingi ya demokrasia lakini pia haki ya kupigania kufanya shughuli za siasa ingawa si kwa mapambano.
Hata hivyo, pamoja na maonyo hayo dhidi ya operesheni hiyo bado chama hicho kimeendelea kusisitiza operesheni hiyo inayotarajiwa kuanza nchi nzima Septemba mosi kuwa itaendelea kutekelezwa.
Ukweli ni kwamba, suala hilo linahitaji kutatuliwa kwa kuzingatia busara kwa pande zote mbili kupeana nafasi ya kusikilizana ili muafaka wenye maslahi ya watanzania upatikane.
Kwa hali ilivyo, operesheni hiyo haina ulazima ifanyike kwa kuwa tayari vyombo vya dola vimeshachunguza na kubaini viashiria vya mvunjiko wa amani hivyo ni vyema kwa waanzilishi wa operesheni hiyo kutafuta njia mbadala kufikisha ujumbe wao.
Ikumbukwe kuwa chochote kitachotokea endapo kutatokea ukaidi dhidi ya suala hili, waathirika wakubwa watakuwa ni wananchi hasa akinamama na watoto na wala si hao wanasiasa wanaopiga kelele majukwaani.
Tayari nchi za jirani tumeshajionea mifano namna kutokuwepo kwa uvumilivu katika masuala ya siasa kunavyoweza kuchangia kuvuruga nchi na kuwaangamiza wananchi huku wanasiasa wenyewe wakiendelea kutamba wakiwa na familia zao salama salimini.
Hivyo ni wakati sasa wa wanasiasa wetu nchini kuzungumza lugha moja kwa maslahi ya wananchi waliowaamini na si maslahi yao binafsi kwa kuhakikisha wanafuta Sheria na misingi waliyojiwekea.
Zipo njia nyingi zinazoweza kutumika ili kuifikishia ujumbe Serikali bila kuhamasisha vurugu kwani hata Rais Magufuli ameweka wazi kuwa hakuna mwanasiasa anayezuiwa kufanya shughuli zake za kisiasa cha msingi afanyie katika eneo lake na si kwenda maeneo mengine kuhamasisha uvunjifu wa amani.

Comments

News