AKILI ZA USIKU NA DDALMAS87.
Imamu anapoiba nguruwe!
UKISHANGAA ya Musa utaona ya firauni, kama kuna kitu ni dhambi kubwa katika dini yetu ya Kiislamu na madhehebu ya Kisabato ni nyama ya nguruwe.
Vitabu vyote viwili yaani Biblia na Kuran vyote vinaeleza kuwa mnyama huyo mchafu hapaswi kufugwa wala kuguswa. “Msile wala msiguse mizoga yao, “ kinasema kifungu kimoja cha Biblia.
Lakini katika hali isiyo ya kawaida, majuzi hapa baadhi ya vyombo vya habari vikaja na habari kubwa na ya kuchekesha kwamba aliyekuwa Imamu wa Msikiti wa Kisesa uliopo wilaya ya Magu, mkoani Mwanza, Salum Yusuph alinusurika kuuawa na wananchi wenye hasira, baada ya kukutwa ameiba nguruwe.
Kiukweli ni tukio la kushangaza kama baadhi ya vyombo vya habari vilivyoripoti, kwani kwa mujibu wa imani ya dini ya Kiislamu, inakatazwa ufugaji na matumizi ya nguruwe kwa muumini wa dini hiyo.
Sasa inakuwaje Imamu tena wa msikiti anaenda kuiba nguruwe! Imamu huyo anadaiwa kwamba anaheshimika sana katika wilayani yake anayoishi ya Magu na kwamba alinaswa na kitoweo hicho haramu maeneo ya makaburini akiwa katika harakati za kumchuna baada ya kumchinja tayari kwa kitoweo.
Kitendo hiki kilichofanywa na muumini wa dini hiyo ya Kiislamu kwangu mimi sio cha ajabu, kwani tabia ya wizi ni dhambi, hivyo kwa muumini wa Kiislamu kuiba sio jambo la ajabu kama ana tabia hiyo.
Awashukuru polisi ambao walifika kunusuru maisha yake, la sivyo leo hii Imamu huyo angechomwa moto na wananchi hao wanaodaiwa kuwa na hasira, licha ya kuwa walikuwa wanampa kipigo huku wakicheka.
Sasa hiyo hasira iko wapi wakati walikuwa wanampiga huku wanacheka? Wizi ni tabia ya mtu, hatuwezi kumhusisha mwizi huyo na imani yake ya Kiislamu, hivyo wananchi walitaka kumuua sio kwa sababu ni Imamu wa msikiti bali kwa kuwa ni mwizi ambaye ameiba mali ya mtu.
Aliiba nguruwe wa mtu akaenda kumchuna huko makaburini, jamii ikakasirika baada ya kukamatwa. Hiyo naamini wananchi walitaka kumwadhibu Yusuph ili liwe funzo kwake aache tabia yake ya kuiba mali za watu.
Ajifunze kufanya kazi, hata kama anatumia hicho kitoweo cha kiti moto, hiyo ni dhambi yake mwenyewe kama ilivyo kwa muumini mwingine wa Kiislamu ambaye anashiriki matendo ya uzinifu na uasherati. Nashangaa watu kusoma habari hiyo wakashangaa wakati waumini wote wa dini zote wanashiriki katika kutenda dhambi.
Kuna waumini wa Kikristo hapa pia wana dhambi zao licha yakuwa dhambi ya imamu huyu hata mashetani walishangaa. Unajua kuna dhambi ambazo binadamu anatenda hadi mashetani nao wanashangaa. Kwa sababu kuna dhambi tunazitenda na yeye shetani anakaa kando kwamba hapana yeye hajatufundisha hata kufanya hayo tunayofanya.
Hivyo Yusuph amefanya dhambi ya kawaida ya wizi, yawezekana alikuwa anajiandaa kwenda kuuza nyama hiyo ili ajipatie fedha za kununua chakula. Hakuna mwenye ushahidi kwamba alikuwa anamchuna nguruwe huyo akamfanye kuwa kitoweo.
Kwa kuwa hakuna mwenye uthibitisho huo, tusimhukumu Imamu Yusuph kwamba alikuwa anaenda kutafuna nguruwe, alikuwa anamwandaa ili akamuuze kwani anajua nyama hiyo inapendwa na watu wengi sana. Pole sana Imamu Yusuph kwa kitendo kilichokupata, lakini cha msingi tubu dhambi yako ya kuiba.
Usiibe tena kama ulikuwa na hamu na nguruwe ungeenda tu kumnunua kwenye bucha ili ule kwa raha na familia yako. Angalia sasa umeiba nguruwe, umepigwa na wananchi, umedhalilisha dini yako, yote haya yasingekupata kama ungeenda kununua duka la nyama ya nguruwe ukaenda kula na uwapendao.
Hakuna ambaye angekufuatilia kwani nani anafuatilia kinachopikwa nyumbani kwako? Wengine tujifunze kwa imamu huyu, kuiba kubaya, wenye hamu tukanunue tu na hapo tutafurahia maisha yetu kwa kula kile ambacho roho inataka. Kipenda roho hula nyama mbichi.






Comments
Post a Comment