Nini hatma ya soka Tanzania.
Nini hatma ya soka Tanzania.
KUNA msemo mmoja wa Kiswahili usemao ‘Mficha ugonjwa kilio kitamuumbua’, hivyo ndivyo inavyoelekea kutokea katika soka la Tanzania.
Kwa muda mrefu kumekuwa na ushabiki usiopendeza baina ya mashabiki wa soka kutoka klabu kongwe za Yanga na Simba. Ushabiki ambao huko unakoelekea sasa inaliweka rehani soka la Tanzania.
‘Mchelea mwana kulia atalia yeye’, ndivyo inavyoonekana kuwa kwa Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambayo inaelekea kabisa imeshindwa kushibiti na hata kusimamia kanuni zake yenyewe na sasa kila mtu anafanya anavyotaka.
Hivi sasa viongozi wa soka wanaonesha wazi kutokubaliana na kila linalosemwa na TFF iwe kisheria au kikanuni. Baadhi wameshaingiwa na dhana kuwa wanahujumiwa na shirikisho hilo, hii ni hatari kubwa!
Klabu ya Simba inalia kuhujumiwa na TFF, vilevile Yanga nayo inalia hujuma kwa TFF, ukweli juu ya huu uko wapi kama siyo kutaka kuwahadaa mashabiki na wadau wa huo hapa nchini?
Ni kweli kuna nyakati TFF ilionekana kukengeuka kidogo lakini hiyo haitoshi kuwapa kiburi vyama au klabu kutaka kuharibu taswira ya soka la Tanzania.
Kweli tumeshuhudia mvutano katika suala la kusimamia uchaguzi wa klabu ya Yanga ambao kama siyo busara za viongozi wa shirikisho hilo kuamua bora yaishe kidogo ungetia doa sura ya mchezo huo hapa nchini.
Nani aliyesahau maamuzi ya kizembe yaliyofanywa na TFF kuiruhusu timu ya Azam kwenda nchini Zambia kushiriki michuano ya kirafiki ikiwa katikati ya ratiba ngumu ya Ligi Kuu ya Tanzania, uamuzi uliozua malalamiko toka kwa timu zingine na hata kuathiri michuano hiyo kwa namna moja au nyingine.
Udhaifu wa waamuzi kubwa, je hatua gani zichukuliwe kutatua tatizo hilo.pangua pangua ya ratiba ya ligi je?
Hivyo vyote vinabaki kuwa changamoto kwa chombo hicho na kwa walio chini yake wanapaswa kufuata taratibu katika kudai haki zao.
Lakini ukiangalia kanuni za Shirikisho hilo zinaweka wazi kabisa mipaka ya kutenda na hata kusema kwa viongozi wa klabu wakiwemo pia Maofisa Habari.
Wanatakiwa kuzungumzia masuala ya klabu lakini pale wanapoona haki haitendeki sawa basi wanapaswa kama kuwasilisha malalamiko yao kupitia vyombo husika. Ikumbukwe kisheria haki inaanzia katika vyombo vya shirikisho hilo na chombo cha mwisho kabisa ni Mahakama ya Usuluhishi ya kimichezo ya Kimataifa ‘CAS’ iliyopo FIFA.
Hali iliyoko hivi sasa kuna kila dalili kuwa iwapo hatua hazitachukuliwa kudhibiti yanayotokea hasa yanayofanywa na wakongwe wa soka nchini Yanga na Simba ni dhahiri kutasababisha kulipoteza kabisa soko la nchi hii.
Figisu, fitna na hata ubabe usio na tija kutoka kwa baadhi ya viongozi wa klabu unachafua sura ya soka hili ambalo sito siri kumekuwepo na mikakati ya kulinasua hapa lilipo ili lisonge mbele.
Kiongozi mmoja wa klabu ya Simba (kisheria si kiongozi) aliwahi kutoa kauli za kutatanisha akiituhumu TFF kuihujumu klabu yao. Hakuishia hao akaongeza kuwa kutofanya vizuri kwao kulichangiwa pia na tuhuma za rushwa kutoka kwa klabu pinzani.
Hiyo ni kauli nzito na toka itolewe hadharani haijawahi kufanyiwa kazi achilia mbali mhusika kutakiwa kuthibitisha vinginevyo kuchukuliwa hatua. Kimya!
Kama hiyo haitoshi mara kadhaa Ofisa habari wa Yanga, Jerry Muro amekuwa akitoa kauli nzito na zinazoweza kuchochea vurugu miongoni mwa mashabiki wao lakini hakuna hata siku moja amechukuliwa hatua ilihali kanuni na sheria zipo.
Ule msemo wa ‘Unalaumu ulipoangukia na kusahau ulipojikwaa’ ukajitokeza baada ya hivi karibuni klabu hiyo kuimeshutumu TFF kuihujumu katika Michuano ya Kombe la Shirikisho kisa tu Kituo cha Televisheni ya Azam kupewa haki ya kurusha matangazo ya mechi yao dhidi ya TP Mazembe.
Kauli kuwa klabu hiyo iko juu kuliko TFF au CAF inapaswa kupigwa vita na wapenda michezo wote kwani bila tahadhari inaweza kusababisha hasira miongoni mwa mashabiki wao ambao siku zote huamini kila lisemwalo na msemaji wao.
Ukweli unabaki kuwa aidha ni uzembe au uelewa mdogo wa viongozi wa klabu hiyo kufuatia kupuuza kuhudhuria semina elekezi iliyoandaliwa na CAF kwa timu zote zinazoshiriki michuano hiyo, ndiyo hasa iliyosababisha mgogoro na kelele zisizo na tija kwa klabu hiyo.
Lakini kitendo cha klabu hiyo kulazimisha mashabiki wao wakae upande unaotumiwa na mahasimu wao Simba nao ni hatari kwa vile ungeweza kusababisha vurugu kutokana na ukweli kuwa klabu hizo haziivi chungu kimoja kwa sasa.
Yote hayo yamesababishwa na wasemaji wao ambao sasa dhana ya chuki miongoni mwa mashabiki wao inashamiri kadri siku zinavyokwenda tofauti na hapo zamani kwamba upinzani wao ulikuwa ni ndani ya mchezo tu.
Kuna hatari kubwa ule uhasama wa kisiasa ukahamia katika michezo ambapo watu wanaweza kushindwa kusaidia na hiyo inaweza kuwa hatari kubwa na hata mustakabali wa soka.
Nani asiyejua kama toka enzi klabu hizi zilikuwa zikishirikiana kwa masuala mengi tu lakini upinzani ukabaki ndani ya uwanja tu. Lakini leo hali ni tofauti.
Wasemaji hao ndiyo wanaopandikiza chuki miongoni mwa mashabiki wa klabu hizi ambazo ndizo zilizobeba taswira kubwa ya soka la nchi hii.
Hali ya kuwadekeza ndiyo hii sasa imefikia hatua hata kutoa matamshi makali kwa vyombo vilivyo juu yao achilia mbali utovu wa nidhamu lakini pia kuchochea chuki kati ya mashabiki na taasisi hiyo. Hali hiyo lazima idhibitiwe.
Suala la kulazimisha mashabiki waingie ndani ya uwanja bure nalo halina mashiko kwavile si kwa wapinzani wao tu bali hata wao haliwapi faida zaidi ya kuwatia hasara kwani wamelazimika kulipa gharama za ziada bila ya kuingiza fedha kupitia mchezo huo.
Ni lazima kupitia mchezo huo CAF, FIFA, TFF, Uwanja wapate mgao wao achjilia mbali Setikali nayo kujipatia kodi.
Ikumbukwe soka ni uwekezaji na ikizingatiwa kuwa chanzo kikubwa cha mapato cha klabu nyingi ikiwemo Yanga ni kutokana na mapato ya mlangoni. Kupitia mechi hiyo ni dhahiri ingeingiza kiasi kikubwa cha fedha. Kama hawakutumia mchezo huo kujipatia fedha watatumia mchezo gani mwingine? dhidi ya Toto au Kagera Sugar?
Kuzomea au kushangilia ni sehemu ya ladha ya ushangiliaji na haiwezekani mechi ifanyike kusiwe na kelele za aina hiyo cha msingi zisipitile kiwango.
Yanga walipaswa kufahamu ili kuzuia hali hiyo wakupaswa kucheza soka zuri kwani kupitia hilo wanaweza kumbadilisha adui yao akawashangilia.
Hali kama hii iliachwa ikaota mizizi sasa athari zake zinaonekana. Kama Yanga wasingeishangilia Stella Abdijan mwaka 1993 na kuiunga mkono TP Mazembe mwaka 2011 ilipokuja kucheza na Simba huenda haya yasingetokea.
Kweli ni aibu klabu za Tanzania kukosa uzalendo na kuzisaidia timu kutoka nje. Nchini Misri kuna upinzani wa jadi kati ya klabu za zamalek na Al Ahly lakini hata siku moja huwezi kuona mojawapo ya kabu hizo ikiisapoti timu ya nje inapokwenda kucheza nchini. Hili ni suala la kujifunza kwakweli.
Hiyo inaonesha dhahiri sapoti wanayopewa timu pinzani na moja kati ya klabu za hapa nchini yana athari kwa timu za nchini.
Lakini iwapo vyombo vinavyosimamia mchezo huu vikiwa dhaifu na kukubali kupandwa kichwani na klabu zake ni dhahiri watayumba na sana sana kuliyumbisha soka hili.






Comments
Post a Comment